Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dodoma
CHAMA cha Mapinduzi CCM, kimetoa tathmini ya kampeni ya Chama hicho kwa zaidi ya siku 25 zilizopita na kusema endapo
uchaguzi mkuu ungekuwa umefanyika Septemba 23, mwaka huu mgombea wao kwa nafasi ya Rais Dkt. John Magufuli angeshinda kwa asilimia 89.5 .
Akizungumza Mkoani Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Humphrey Polepole amesema hadi sasa hali ya kampeni ndani ya Chama chao inaendelea vizuri ikiongozwa na Dkt. Magufuli.
Amesema, kampeni inayoongozwa na Dkt. Magufuli Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan, Makada mbalimbali na makada waandamizi wameendelea kujenga hoja na kuzungumza sera za chama kwa watanzania.
Polepole amesema pia kampeni zinazoendelea kwa ngazi ya Mikoa ,Wilaya, Majimbo na Kata zinaendelea vizuri.
“Niendelee kuwashukuru na kuwapongeza watanzania kote nchini kwa ushirikiano wao,kwa mapokezi yao makubwa kwa upendo waliotuonyesha katika mikoa hii tuliyoyopita, Dkt.Magufuli hatawaangusha mnampa deni kubwa,” amesema na kuongeza.
“Kuna wakati mwingine tumefanya mikutano saa 12 asubuhi unakuta viwanja vimejaa watu wakimsubiri Dkt.Magufuli mmetupa deni tunawahakikishia tutaendelea kuwa wanyenyekevu na watiifu,watumishi wema kwa nchi yetu ya Tanzania,” amesema.
Polepole amesema misingi ya sera nzuri mipango imekaa vizuri ambayo ipo katika ilani ya chama chao.
“Kwa Zanzibar napo tunaendelea vizuri sana ambapo mgombea wa Urais wa Zanzibar,Hussein Ali Mwinyi nae anaendelea vizuri na kampeni ambapo tayari ameshafanya mikutano Unguja,Pemba na maeneo mbalimbali na mwitikio uliopokelewa na wazanzibar umetupatia deni,tunachoahidi ni maendeleo makubwa kwa haraka katika mtindo wa kiuongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa kutetea haki kwa maslahi ya wanyonge na kupeleka maendeleo na maslahi mapana ya wazanzibar,” amesema.
Aidha Polepole amesema, wamejipanga kwa awamu ijayo kwani awamu ya pili wameweza kufanya mizunguko ya kampeni na kugusa nchi nzima kwa maeneo tofauti tofauti katika msafara wa Dkt. Magufuli, Mama Samia pamoja na Makada wandamizi.
Amesema katika kampeni hiyo wameweza kufanya kwa kutumia magari na kupita katika barabara ambazo zipo katika kitabu cha ilani yao na sasa wameweza kuongeza nguvu kwa kutumia helkopta ambayo itawafikisha katika maeneo ambayo hayafiki
kwa urahisi.
More Stories
Wananchi Kiteto waishukuru Serikali,ujenzi wa miundombinu ya barabara
Watoto 61 wenye mahitaji maalum washikwa mkono
Mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi,adaiwa kubakwa na baba wa kambo