November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Majaliwa ahimiza wabunge,jamii kushiriki michezo kujenga afya

Na Joyce Kasiki,Timesmajira,Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasisitiza wabunge na jamii kwa ujumla kushiriki katika michezo ili kujenga na kuimarisha miili yao kwa lengo la kujiepusha na mamba mbalimbali ikiwemo magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Ameyasema hayo katika bonanza la wabunge lililofanyika katika viwanja vya shule ya msingi na sekondari ya John Merlin ya jijini Dodoma huku akisema bonanza hilo litakiwa likifanyik mara kwa mara.

“Michezo ni muhimu zaidi kwa sababu inatufanya tuwe na afya bora zaidi na pia michezo inasaidia watu kukutana pamoja na kuimarisha undugu, kujenga urafiki pamoja na kukuza vipaji. “amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Spika wa Buge kwa ubunifu wake wa kuanzisha bonanza hilo ambalo litakiwa likifanyika mara akwa mara.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia amesema Bunge Bonanza litakuwa linafanyika mara nne kwa mwaka lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi waone umuhimu wa  wa kushiriki katika kufanya mazoezi ili jamii iweze kuwa na afya bora zaidi.

Naye, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Katibu wa Michezo wa Baraza hilo  Nassor Salim Ali (Jazeera)  amesema kwa upande wa Zanzibar nao Baraza litaendelea kushirikiana na Bunge ili kudumisha undugu kupitia michezo pamoja na shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Awali, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Festo Sanga amesema pamoja na mambo mengine bonanza hilo limeanzishwa ili kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluh Hassan ambaye amekuwa akiihamasisha jamii kushiriki katika kufanya mazoezi kwa ajili ya kuupa mwili afya na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Timu zilizoshiriki katika bonanza hilo ni timu ya Bunge na ya watumishi wa Bunge ambapo timu ya Bunge ilipata kombe la mshindi wa jumla baada ya kuishinda timu ya Watumishi wa Bunge katika michezo mingi iliyochezwa  siku hiyo.

 Michezo hiyo ni  pamoja na mpira wa miguu, mpita wa wavu, mpita wa meza, mpira wa mikono, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, kula chakula, kunywa soda, kuvuta kamba na kurusha tufe.