January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pinda ataka kaulimbiu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ihusianishwe na kuenziwa kwa mwalimu Nyerere

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, amesema Kauli mbiu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ‘Tumerithishwa, Tuwarithishe’ ina mantiki wakati huu ambao taifa linaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Amesema kuna umuhimu wa viongozi waliopo kwenye uongozi, kuwarithisha vijana mazuri waliyorithishwa kutoka kwa viongozi wengine akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, hususan uadilifu na kukataa vitendo vya rushwa na ufisadi.

Hayo ameyasema wilayani Butiama mkoani Mara, kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 100 ya Hayati Mwalimu Nyerere, iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, yakiwa na ujumbe: “Tumuenzi kwa kudumisha amani, umoja, uhuru na kazi.”

Amefafanua kuwa: “Tunapokuwa tunatazama dhana ya kurithishwa na kurithisha, lazima awamu zote zilizopita na zilizopo, tuyachukue na tuone ni kitu kinachomhusu mwingine.”

Akizungumzia suala la malezi, Pinda amesema suala hilo lina nafasi kubwa ya kumpika kiongozi kuanzia ngazi ya familia hadi katika uongozi wa umma, kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere.

Amesema Uviko-19 bado ipo na kuhimiza chanjo huku akisisitiza kiwa Sensa ya Watu na Makazi, kila Mtanzania ana wajibu wa kuhesabiwa ifikapo Agosti, mwaka huu.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amesema wizara imeandaa namna ya kumuenzi Hayati Mwalimu Nyerere kwa kuinua sekta ya utalii nchini kupitia nyumba za makumbusho.

Amesema katika tathimini iliyofanywa, wizara imebaini zipo hatua zimechukulia katika kuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere kwa kuanzishwa makumbusho ya Mwalimu Nyerere.

Naye, Kiongozi Mkuu wa Ukoo wa Burito unaolea familia 13 ikiwemo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, Chifu Japhet Wanzagi, ameshauri kujengwa sanamu ya Mwalimu Nyerere kwenye mzunguko mmojawapo Musoma Mjini.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, John Butiku, naye ametoa rai kwa Watanzania kuwa kwenye chaguzi zote zijazo wachague viongozi bila rushwa.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeshiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ya miaka 100 ya Hayati Mwalimu Nyerere, ikiongozwa na Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Sylivester Mushi ambaye alimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda.

TAWA imeshiriki kwa kuweka banda la maonesho katika Uwanja wa Mwenge, Butiama, ambapo pamoja na mambo mengine viongozi na wananchi walifika na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhifadhi.