May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PIC yataka serikali ifanye tathimini ya madeni chechefu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji ya Umma (PIC) imesema,ipo haja kwa Serikali kufanya tathimini ya madeni chechefu ya baadhi ya mashirika na kubadilisha kuwa mtaji kwani vitabu vya baadhi ya mashirika ,vimeathiriwa na  uwepo wa madeni hayo.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma kufuatia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hersabu za Serikali kwa mwaka ulioishia Juni 30,2022,Mwenyekiti wa Kamati hiyo Deus Sangu amesema  jambo hilo ni hatari kwa misingi ya kibiashara na ukuaji wa Shirika kwa ujumla.

Mwenyekiti huyo ametolea mfano wa hesabu wa vitabu vya DAWASA vinaonesha vinaathitiwa na deni la shilingi bilioni 47 ambalo wamelirithi kutoka DAWASCO lakini pia Mfuko wa Self Microfinance una deni la shilingi bilioni 6 .3 ambalo imelirithi kutoka walipounganishwa na UTT Microfinance.

Kufuatia hali hiyo amesema,ipo haja ya madeni haya kupitiwa upya na kuona kama kuna uwezekano wa kupeleka kutoka kwenye deni na kuwa mtaji.

“Kwa msingi wa mambo haya kamati inatoa mapendekezo ambayo iwapo bunge litaridhia yanaweza kutatua changamoto zilizopo katika Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.”amesema Sangu na kuongeza kuwa

“Bunge linaazimia kwamba Sheria ya Msajili wa Hazina sura ya 370  irekebishwe ili kuweka bayana mfumo wa taasisi zote zinazopata faida ziwajibike  kisheria kuchangia katika mfuko Mkuu wa Serikali,na

Serikali iongeze msisitizo kwa taasisi zinazotumia mtaji wa umma ili zitekeleze wajibu wa kuchangia katika mfuko Mkuu wa Serikali ,

“Na pale ambapo itatokea kutokuzingatiwa kwa wajibu huo adhabu na hatua nyingine stahiki zichukuliwe katika kukazia utekelezaji maana kwa ilivyo sasa taasisi inaweza isipeleke gawio lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.”

Kuhusu utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini Sangu amesema,Bunge linaazimia kwamba Serikali iweke utaratibu wa kufanya tathimini ya mara kwa mara  ya taasisi za umma ili kubaini zinazohitaji ruzuku ,taasisi za umma zinazotumika mtaji wa umma na  zinapatiwa mtaji wa Serikali zikifikia kiwango cha kujitegemea zipewe muda mahususi na kuanza kujitegemea.

Aidha  Mqwenyekiti huyo amesema kuwa Bunge linaazimia kufanyika kwa  marekebisho ya Sheria ya Msajili wa Hazina sura 370  ili kumuongezea nguvu Msajili wa Hazina kwa lengo la kufuatilia na kuziwajibisha Bodi zinazoshindwa kuzingatia vigezo.