December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pesapal Tanzania yapata leseni ya TCRA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar

KAMPUNI ya huduma za malipo ya fedha kidijitali ya Pesapal Tanzania imepiga hatua muhimu ya kufanya biashara hiyo nchini baada ya hivi karibuni kupata leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Ili kuwa mtoa huduma za malipo ya kidijitali nchini, kampuni hiyo pia inahitaji baraka za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa biashara hiyo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari ya Julai 28, mwaka huu,Pesapal ilisema imepewa leseni aina ya National Application Service (AS) na TCRA ambayo itaiwezesha kutoa huduma za malipo ya kidijitali kwa kampuni na watu binafsi.

“Kupenya kwa huduma za kimtandao nchini kulifikia asilimia 85 mwanzoni mwa mwaka 2020. Kutokana na ukuaji wa miamala ya kibiashara mtandaoni, leseni hii inaimarisha dhamira ya Pesapal kutoa suluhishi nafuu, bunifu na rahisi kwa watumiaji na biashara ndogo ndogo,” amesema Meneja Mkuu wa Pesapal Tanzania, Bupe Mwakalundwa.

Ili kuweza kuwahudumia wateja wake vizuri, kampuni hiyo imesema itashirikiana na wadau mbalimbali kuchochea na kuongeza huduma shirikishi za kidijitali nchini. Kwa njia hiyo, itakuwa rahisi kwa wafanyabiashara kupokea malipo kupitia mifumo tofauti na kuwawezesha watumiaji kulipia huduma na bidhaa kwa wepesi.

Kampuni ya Pesapal ilianzishwa rasmi mwaka 2009 na sasa hivi inafanya biashara katika nchi sita barani Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Rwanda na Zimbabwe. Shughuli zake kubwa ni kusaidia kuchakata biashara kwa njia ya mtandao na mauzo kidijitali.

Programu ya Sabi ya Pesapal inamwezesha mfanyabiashara kufanya biashara kwa mtandao pamoja na malipo

“Pesapal usaidia watu na makampuni ya biashara kufanya na kupokea malipo pamoja na kuyasimamia kikamilifu. Pesapal ushirikiana na benki, kampuni za simu na kampuni za kadi za mikopo kuwawezesha wateja wake kufanya malipo kwa njia mbalimbali,” kampuni hiyo ilifafanua katika taarifa yake.

Aidha, kupatikana kwa leseni ya TCRA kunadhihirish dhamira yake ya kuendeleza malipo kwa njia za kidijitali barani Afrika. Maono ya kampuni hiyo ni kuwa njia salama zaidi na rahisi ya kulipa na kulipwa kwa wateja wake.

Shughuli za Pesapal nchini kunatarajiwa kusaidia sana ajenda ya kitaifa ya kuendeleza huduma jumuishi za kidijitali na kifedha jambo ambalo imefanikiwa kulifanya kwa mafaniko makubwa katika nchi zote inakofanya biashara barani Afrika.