March 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PDPC yazitaka taasisi za umma,binafsi kujisajili

*Ni zile zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi

*Yatoa muda wa mwisho usajili Aprili 30,2025

 Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Imeelezwa kuwa taasisi 2000 zinazohusika na ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi kati ya 140,000 nchini,zimejisajili kwenye Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi(PDPC).Huku Mkoa wa Mwanza ukiwa ni moja ya Mikoa ambayo usajili wake upo chini ukiwa na taasisi 20 tu zilizojisajili mpaka sasa.

Kutoka na zoezi hilo kuwa na kasi ndogo,PDPC imetoa wito kwa  taasisi zinazohusika na ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi, kujisajili  kwenye Tume hiyo, kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na maandalizi muhimu ya kazi wanazofanya na kuhakikisha  wanafahamu wapi panaweza kuwa na mwanya taarifa hizo kutumika vibaya.

Hayo yameelezwa Machi 22,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC,Dkt.Emmanuel Mkilia,wakati akifunga warsha ya siku moja ya  kuwajengea uelewa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza juu ya dhana mzima ya ulinzi wa taarifa binafsi,iliofanyika mkoani hapa,ambapo amesema baada ya Rais Samia  Suluhu Hassan,kuzindua Tume hiyo,aliitaka kuhakikisha taasisi nyingi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi  zisajiliwe.

Mkilia, amesema wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi kujisajili kwao ni kuonesha msimamo na  uimara wa kuhakikisha kuwa taarifa zile zitatumika  kwa ajili ya matumizi kusudiwa na si vinginevyo.

“Wakuu wa taasisi zote za Serikali na Binafsi, kuhakikisha taasisi zao zimejisajili,ambapo zoezi la usajili limesogezwa.mpaka Aprili 30,2025 kwani awali lilikuwa likamilike Desemba 30,2024, na baada ya muda kupita wahusika watakuwa wanatenda kosa.Taasisi kubwa ni pamoja na za kifedha,kampuni za simu,kilimo,ufugaji wa samaki,usafiri na usafirishaji  huku taasisi ndogo ni pamoja na nyumba za kulala wageni huko pote watu wanajaza taarifa binafsi,”.

Pia amesema,taasisi hizo  kujisajili PDPC, itawezesha utaratibu  wa mifumo yote ya Serikali na binafsi kusomana pamoja na Tume kusimamia jukumu waliopewa kisheria la kuhakikisha kwamba taarifa binafsi zinatumiwa kwa utashi na makundi kusudiwa na yanazingatia usalama.

Hata hivyo,amesema,mifumo ikisomana mtu atahudumiwa kutokana na utambulisho wake na  kila mwananchi atakuwa na uwezo wa kujua taarifa zake zimetumika wapi kupitia Jamii Portal,ambayo inamruhusu kila mtu  kuangalia taarifa zake zilitumika wapi na kwanini na je aliridhia au aku ridhia na  kama taarifa zilitumika sehemu ambapo akurudhia ataiona Tume.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji kutoka PDPC, Mhandisi Stephen Wangwe,amesema taasisi hizo zinaweza kujisajili kwa njia  mtandao,na mpaka sasa wameisha pokea malalamiko  takribani 60 kati yao  mengi  yenye hali ya udhalilishaji.

“Mwananchi anahitaji kukopa kupitia wakopeshaji wa mitandaoni wa “apps”ambazo lazima upite hatua fulani ili iweze kupata huduma,katika hatua anazopita kuna sehemu mtumiaji anaulizwa unaturuhusu tumtumie orodha yako ya namba  zilizopo kwenye simu yako”phone book”,wengi wamekuwa wakitiki sasa wakati  wa malipo mtoa huduma anapeleka ujumbe wa kumdhalilisha yule mtu kwenye orodha ile.Tumeshirikiana na Benki Kuu ya Tanzania(BOT),Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na vyombo vya ulinzi na usalama kuzifutia usajili taasisi zote zinazofanywa huduma hizo na tunatoa wito kwa watu kuwa makini na kile ambacho  tunaomba,”.

Naye Mkuu wa Uhusiano  na Mawasiliano kwa Umma wa PDPC, Innocent Mungy,amesema ulinzi wa taarifa binafsi ni muhimu katika uchumi wa kidigitali,kwani  katika uchumi huo inahitajika imani kuweza kufanya biashara kwa njia ya mtandao.

“Mfano kuuza kwa bidhaa kwa kutumia mitandao,kufanya shughuli za kibenki(fedha), kupitia mitandao,kunapokuwa na ulinzi wa taarifa binafsi watu wanaingia kwenye biashara ya mtandao kwa sababu wanaimani kwamba taarifa zao zipo salama, na wanaweza kutumia kadi zao za benki  na kufanya miamala bila ya wasiwasi,” amesema Mungy.

Mungy,amesema suala jingine la ulinzi wa taarifa binafsi ni kutengeneza fursa za kiuchumi kwa njia ya kidigitali ambazo zamani ilikuwa lazima mtu aende mahali  kufanya biashara au kununua bidhaa.

“Lakini sasa hivi unatumia mitandao ya kijamii mtu anaweza akaagiza bidhaa siyo tu hapa nchini bali nje ya nchi na bidhaa ikamfikia mahali alipo, pia kuwezesha malipo mbalimbali ambayo yanafanyika katika uchumi wa kidigitali.Mtu anapokuwa na uhakika wa huduma zinazotolewa na taarifa zao kuwa salama ni rahisi kufanya uhamishaji wa fedha na kukuza uchumi wa nchi kupitia kidigitali,”.