Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
KOCHA mkuu wa la timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni ‘Beach Soccer’, Boniface Pawasa amesema kwa sasa kazi kubwa iliyo mbele yake ni kuhakikisha wanafanikisha mikakati yao kuwa na kikosi bora inafanikiwa kabla ya kuanza rasmi kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (BSAFCON 2021) zitakazofanyika kuanzia Mei 23 hadi 29 nchini Senegal.
Timu ya Tanzania ilifanikiwa kufuzu fainali hizo baada ya kupata ushindi wa jumla wa goli 12-9 wakifanikiwa kushinda goli 8-3 katika mchezo wa kwanza na kufungwa goli 6-4 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Aprili 3 kwenye fukwe za Coco.
Kilichowasaidia kufuzu kucheza fainali hizo ni mbinu waliyoitengeneza katika mchezo wao wa kwanza ambao ulikuwa wa ugenini jambo lililowapa wepesi katika mchezo wao wa pili ambao ulikuwa mgumu zaidi.
Kocha huyo ameuambia Mtandao huu kuwa, ili kuhakikisha wanafanikiwa mkakati wake waliandaa programu ya mazoezi ambayo imegawanyika katika sehemu tatu ambapo wiki ya kwanza ilikuwa kwa ajili ya kujenga utimamu, wiki ya pili itabeba zaidi mambo ya kiufundi huku ile ya tatu ikihusisha zaidi mechi za kirafiki.
Toka wameingia kambini hadi sasa wachezaji wake wanaendelea kuimarika na kuwa bora na wameanza kutekeleza awamu ya pili ambayo itajikita zaidi kwenye mbinu za kiufundi, ujanja na ubunifu kwani utawasaidia kufanya vizuri katika mechi zao.
Pawasa amesema, baada ya hapo wiki ya mwisho itakuwa ya mechi za kirafiki ambapo watacheza mechi mbili dhidi ya mabingwa watetezi Senegal lakini wapo kwenye mpango wa kutafuta mechi nyingine ili kuweza kubaini mapungufu yao na kuiyafanyia kazi haraka kwani mkakati wao ni kufanya vizuri katika michuano hiyo.
“Katika mashindano haya tunakwenda kukutana na timu ngumu za bora hivyo ili waweze kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita ni lazima tufanye maandalizi yatakayotuwezesha kuwa bora zaidi ili kuweza kupambana na vigogo wengine waliofuzu kwenye fainali hizi,” amesema kocha huyo.
Hii ni mara ya pili mfululizo Tanzania inafuzu kucheza fainali hizo baada ya mwaka 2018 kufanikiwa kufanya vizuri baada ya kudika nafasi ya nane katika ya nchi 52 katika viwango vya Afrika na dunia.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM