Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu waziri wa wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul, amesema matunda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kukubali kuwa mwenyeji wa mashindano ya Mataifa Barani Afrika kwa Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu (CANAF) yameanza kuonekana kwa watanzania kujivunia mchezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu (Tembo warriors) Frank Ngailo, kwa mafanikio aliyopata kuanzia katika mashindano hayo kwa kuibuka na tuzo ya mchezaji bora, mchezaji mwenye nidhamu lakini pia kupata nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Izmir BSB nchini Uturuki.
Mhe. Gekul ameyasema hayo leo Januari 17, 2022 alipokuwa anamuaga mchezaji huyo aliyeambatana na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu (TAFF) akiwemo mwenyekiti wa Bodi ya TAFF Mheshimiwa Riziki Lulida, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA).
“Sisi tumekuja hapa kuwakilisha umoja wetu, kwamba katika mafanikio yako haya na sisi tunafurahia kama watanzania tunajivunia tunahubiri kwamba michezo ni ajira, maana yake tunaonyesha sasa kwa vitendo kwa wewe kuonyesha jitihada zako lakini pia wakati tunafanya mashindano ulikuwa mchezaji bora, mchezaji mwenye nidhamu umetubeba watanzania na umetangaza nchi yako vizuri sana, unapokwenda huko mwenyezi Mungu akutangulie, kwa kuwa na sisi tunakuombea tunaamini utafanikiwa, ili umalize hizo siku zako 15 za majaribio na mechi 4 unazoenda kucheza,” amesema Mhe. Gekul.
Kwa upande wake mchezaji Ngailo ameishukuru Serikali na uongozi wa TAFF, kwa kuwa naye bega kwa bega kuhakikisha suala lake linafanikiwa, na kuahidi watanzania kufanya vizuri katika majaribio hayo kwani ni ndoto aliyokuwa nayo muda mrefu kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
“Cha kwanza nipende kumshukuru mwenyezi Mungu kwa yote aliyoyafanya mpaka tumeweza kukusanyika mahali hapa, pia nipende kushukuru uongozi wa Serikali uliopo hapa kwa kuwa nami bega kwa bega mpaka nimeweza kufanikiwa, naahidi kwamba nitaenda kufanya vizuri kwani ni moja ya ndoto zangu kucheza nchi za nje ili kuweza kuisaidia nchi yangu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa,” alisema Ngailo.
Aidha Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limekabidhi kiasi cha fedha shilingi milioni mbili ikiwa ni posho ya mchezaji huyo itakayomsaidia atakapokuwa nchini Uturuki.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania