July 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Patali akabidhi ambulance Santilya,kuokoa wajawazito

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya.

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida Patali, amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) kwa Kituo cha Afya Santilya, hatua inayotarajiwa kupunguza vifo vinavyotokana na ucheleweshaji wa huduma za dharura, hususan kwa wajawazito, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika Julai 9, 2026, Patali alisema serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza magari ya wagonjwa katika jimbo hilo, ambalo sasa lina ambulance tano licha ya mahitaji kuwa makubwa kutokana na ukubwa wa eneo na idadi ya wananchi.

Alisema Jimbo la Mbeya Vijijini lina kata 28 na wakazi zaidi ya 470,000, huku magari mengi ya wagonjwa yaliyopo yakiwa katika hali isiyoridhisha.

“Nimekuwa nikishawishi kwa nguvu zote Serikali iongeze magari ya wagonjwa na kusema kwa sasa tuna ambulansi tano tu, na kati ya hizo mbili pekee ndizo zipo katika hali nzuri kutokana na jiografia ya jimbo letu na idadi ya wananchi, bado mahitaji ni makubwa,” alisema Patali.

Alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kuidhinisha upatikanaji wa gari hilo, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof.Shemdoe, kwa ushirikiano alioutoa katika kufanikisha upatikanaji wa ambulance hiyo.

Patali alisema ambulance hiyo haitawahudumia wakazi wa Kata ya Santilya pekee, bali wananchi wote wa Tarafa ya Isangati na maeneo ya jirani.

“Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia akina mama wajawazito wakijifungulia njiani kutokana na kukosekana kwa usafiri wa dharura, hali iliyokuwa ikiweka maisha ya mama na mtoto hatarini hivyo tunaamini ambulance hii itasaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali imewekeza zaidi ya shilingi milioni 300 kununua gari hilo, akisisitiza kuwa uwekezaji huo una thamani kubwa kwa kuwa unalenga kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, mkazi wa Kitongoji cha Ivugula, Kata ya Santilya, Esther Mboma, alisema wananchi wamekuwa wakipoteza ndugu zao kutokana na kuchelewa kufikishwa hospitalini.

“Juzi tu tulimpoteza mama mmoja aliyekuwa amejifungua salama, lakini alipokuwa akikimbizwa Kituo cha Afya Ilembo alifariki njiani. Tumepoteza wanawake wengi kwa sababu ya changamoto ya usafiri wa dharura. Tunamshukuru Mbunge Patali kwa kutuletea ambulance hii. Sisi wanawake tuko tayari hata kushiriki kuboresha barabara ili gari hili liweze kupita wakati wote,” alisema.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Dkt. Erasto Rite, alisema Kituo cha Afya Santilya ni miongoni mwa vituo sita vya afya vinavyomilikiwa na halmashauri hiyo na kinahudumia wakazi 17,624 wa Tarafa ya Isangati.

Alisema kabla ya kupatikana kwa ambulance hiyo, kituo hicho kilitegemea gari la Kituo cha Afya Ilembo kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 20, hali iliyokuwa ikisababisha ucheleweshaji wa huduma za dharura kwa wajawazito na wagonjwa wengine.

Dkt. Rite pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, kwa usimamizi wake uliochangia kuboresha utoaji wa huduma za afya katika halmashauri hiyo.

Alisema ujio wa ambulance hiyo utapunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika na kuboresha upatikanaji wa huduma za rufaa kwa wananchi wa Santilya na maeneo jirani.