Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Dkt. John Pallangyo, ameibana Serikali kuhusiana na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika vitongoji 37 vya jimbo hilo, ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo muhimu.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo katika kipindi cha maswali na majibu, Dkt. Pallangyo alihoji:
“Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA katika vitongoji 37 ambavyo vipo gizani katika Jimbo la Arumeru Mashariki?”
Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alieleza kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lina jumla ya vitongoji 330, ambapo kati ya hivyo, vitongoji 284 tayari vimeunganishwa na umeme, huku 17 vikiwa kwenye hatua ya utekelezaji kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification IIB) na Mradi wa Kupeleka Umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA).
Aidha, Naibu Waziri Kapinga alibainisha kuwa kwa vitongoji 29 vilivyosalia, tayari Serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya kupata wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo kupitia Awamu ya Pili B ya Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini (HEP IIB).
“Kukamilika kwa miradi hii kutawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Arumeru Mashariki kufikiwa na huduma ya umeme,” alisema Kapinga kwa kusisitiza.
Katika swali la nyongeza, Dkt. Pallangyo aliitaka Serikali kueleza ni lini kitongoji cha Seneto, kilichopo kwenye Kata ya King’ori, kitapatiwa umeme wa uhakika ili kusaidia kazi za taasisi ya COICA ambayo imefungua mitambo ya kusafisha maji yenye kiwango kikubwa cha floridi yanayotoka katika vyanzo vya Mlima Meru.
“Kata za King’ori, Reguruki, Ngarenanyuki na Nangabobo zinapata maji kutoka misitu ya Mlima Meru lakini maji hayo yana kiwango kikubwa cha floridi. Taasisi ya COICA imejitolea kufunga mitambo ya kuyasafisha, je Serikali iko tayari kupeleka umeme wa uhakika kusaidia shughuli hii?” alihoji Dkt. Pallangyo.
Akijibu, Kapinga alikiri kuwa suala hilo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu na Mbunge huyo, na kuongeza kuwa tayari Meneja wa TANESCO Wilaya ya Arumeru Mashariki amepewa maelekezo ya kutenga bajeti kwa mwaka ujao wa fedha ili kuhakikisha kitongoji cha Seneto kinapata umeme wa uhakika.
“Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa jambo hili linatekelezwa kuanzia mwezi Julai. Nimemwelekeza Meneja wa TANESCO kuhakikisha hatua hiyo inafikiwa kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wa Seneto kupata maji safi kupitia mitambo ya COICA.”
Alisema, Serikali imeonesha dhamira ya kukamilisha miradi ya umeme katika maeneo yote yaliyosalia ndani ya Jimbo la Arumeru Mashariki, huku Mbunge Dkt. Pallangyo akiendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma stahiki.
.
More Stories
Sheikh Ponda akabidhiwa kadi ya heshima ya Maalim Seif
Sheikh Ponda kutua rasmi Act Wazalendo
Puma Energy Yazindua Mradi wa Umeme wa Jua kwa Kiwanda cha Alliance One