December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PAC yafurahishwa matumizi bora ya uwekezaji Kiwanda cha nyama

 NA MWAINDISHI WETU, MOROGORO

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee-PAC) imeipongeza Serikali kwa kuridhia uwekezaji uliofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye Mradi wa Uendelezaji wa shamba (Rachi) ya kunenepesha Mifugo na Machinjio ya kisasa wa Nguru Hills Ranch ulioko Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa PAC Japhet Hasunga kutembelea kiwanda hicho kwa nia ya kukagua uwekezaji uliofanywa na PSSSF kwenye Mradi huo.

“Kamati yetu ni kuangalia thamani ya fedha, matumizi ya fedha, hivyo tuna wajibu wa kuhakikisha hizo fedha kama kweli zimetumika na uwekezaji wake una tija, niwapongeze kwa uwekezaji huu, ukiangalia manufaa ya kiwanda kwa jamii inayozunguka eneo hili, ajira, kwakweli ni mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.” Alifafanua Mhe. Hasunga.

Mradi wa Machinjio ya Nguru Hills unaendeshwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Wabia wenza ambao ni Kampuni ya Eclipse Investiment LLC na Kampuni ya Busara Investment LLP

Akizunguzma mara baada ya kutembelea Mradi huo Mjumbe wa Kamati Mhe. Issack Kamwelwe aliipongeza PSSSF kwa uamuzi wa kuingia ubia na wawekezaji wa nje.

“Huu ni mfano mzuri kwa wengine na muutangaze, Arabuni huwezi kwenda kuwekeza bila ya kuwa na mwenyeji wa pale, hapa nchini kuna baadhi ya wawekezaji wamewekeza bila ya kuwa na Mtanzania ndani ya uwekezaji huo, niwapongeze sana PSSSF kwa kutoka na kuungana na wawekezaji wa nje.” Alipongeza Mhe. Kamwelwe.

Alisema kazi kubwa iliyo mbele ni kutangaza kwenye soko (marketing). 

“Kwa ubora wa nyama tuliyoiona hapa, mimi makazi yangu ni Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma tuelekezane ili na mimi nianze kutumia nyama ya kutoka hapa.” Alisema Mhe. Kamwelwe.

Akiwakaribisha wajumbe wa Kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt.  Aggrey Mlimuka alisema Machinjio ya Nguru Hills hutumia malighafi kutoka kwa wafugaji walioko wilaya ya Mvomero na maeneo jirani

Alisema Kiwanda hununua Ng’ombe kutoka kwa wafugaji, kisha hukaa nao kwa muda ili kuwanenepesha kufikia kiwango kinachohitajika.

“Ng’ombe wa chini ya Kilo 300 hachinjwi na akinunuliwa lazima atunzwe kwa nia ya kumnenepesha hadi afikie kiwango hicho.” Alisema.

Alisema wao kama Bodi wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa kwa usimamizi madhubuti katika kiwanda hicho.

Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mradi, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema, PSSSF iliungana na wabia wengine mwaka  2017 ikimiliki hisa asilimia 39% huku wabia wengine wawili wakimiliki jumla ya  asilimia 61%.

Alisema Mradi huo unajumuisha Ranchi ya Mifugo pamoja na Machinjio ambapo eneo lote lina ukubwa wa Hekta 2328 sawa na Mita za Mraba Milioni  23, 280,000 ikiwa na uwezo wa kutunza  Ng’ombe elfu 10,000 na Mbuzi  15,000 kwa wakati mmoja.

Alisema Machinjio hayo yana eneo la Jengo la kiwanda (Utawala), machinjio, eneo la kufungashia (Packeging), maabara, eneo lamkubadilishia nguo na vyumba vya kupozea (cold rooms) na visima vine vikubwa vyenye uwezo wa kuzalisha lita 20,000 kwa saa.

Alisema kwa siku kiwanda kinachinja Ng’ombe 100 kwa siku na Mbuzi 1,000 kwa siku.

“Mpaka sasa kiwanda kimezalisha tani 150 za nyama sawa na N’ombe 1,153 zenye thamani ya shilingi Bilioni 1.59, tuko kwenye hatua za kukamilisha kupata kibali cha 1S0-220000 ili tuwe na uwezo wa kusafirisha nyama kwenye nchi ambazo zinahitaji hati ya ubora ya ukaguzi ubora ISO.” Alifafanua CPA. Kashimba.

Alisema manufaa ya uwekezaji ni kuongeza thamani ya Mfuko kutokana na mapato yatakayotokana na uwekezaji, kuongeza kipato cha wafugaji na wakulima, kuongeza pato la taifa lakini pia kuongeza ubora wa bidhaa za ngozi.

Alisema kampuni ya Nguru Hills Rach inatumia mawakala kukusanya Ng’ombe kutoka kwa wafugaji lakini pia wafugaji moja kwa moja wanaweza kuleta mifugo yao lengo ni kuhakikisha mali ghafi (Ng’omba na Mbuzi) zinapatikana wakati wote.

Alisema Bidhaa zinazozalishwa zinazingatia viwango vya kimataifa kwa kufuata taratibu za HACCP (Hazard Analysis and Critical Control Points) na kwa kufuata misingi ya halal.

Lengo la Kampuni ya Nguru ni kuuza asilimia 80 ya bidhaa zake nje ya nchi na asilimia 20 katika soko la ndani ya nchi.

“Tayari tumepokea oda ya kupeleka nyama iliyogandishwa  tani 54 kwa wiki kwenye nchi za UAE, kwa hivyo tutakapopata tu ISO .” Alibainisha CPA.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita, kuna mabadiliko makubwa ya kisera yaliyopelekea mazingira mazuri ya uwekezaji.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya PAC wakiangalia jinsi nyama inavyochakatwa kwenye Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills, wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Machi 19, 2023.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Mhe. Japhet Hasunga (katikati), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mlimuka (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba wakijadiliana jambo.
CPA Hosea Kashimba akiwatembeza wajumbe wa Kamati kwenye eneo la Machinjio
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC. Mhe. Japhet Hasunga (watatu kushoto) na wajumbe wa Kamati hiyo wakisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Uendeshaji wa Machinjio Eric Cormack wakati Kamati ilipotembelea Rachi na Machinjio ya Nguru Hills.
Meneja Uendeshaji wa Machinjio Eric Cormack akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Bunge ya PAC. kuhusu uendeshaji wa machinjio hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mlimuka (katikati) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya PAC walipotembelea Mradi wa uwekezaji wa Rachi na Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills.
Baadhi ya watendaji wa PSSSF, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha, Beatrice Musa-Lupi (kulia)
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mlimuka (kushoto) Mkurugenzi Mkuu PSSSF, CPA. Hosea Kashimba na Meneja Uhusiano na Elimu Kwa Umma wa Mfuko huo, James Mlowe wakiwasubiri kuwapokea wageni wao (Wajumbe wa Kamati ya Bunge PAC)