Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema Wazanzibari wapo kwenye hatua ya mwisho ya kujikomboa dhidi ya umasikini na madhila yaliyoletwa na watawala waliowatelekeza kwa muda mrefu. Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuhakikisha mabadiliko yanapatikana na sauti ya umma inasikika.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Micheweni, Kaskazini Pemba, Othman alisisitiza kuwa tarehe 29 Oktoba ni siku ya kihistoria kwa wananchi kufanya maamuzi ya kuiondoa CCM madarakani.
Wananchi wa Zanzibar wamechoka na madhila. Leo hii kila mmoja ana kila sababu ya kuwaadhibu watawala waliowaacha bila matumaini. Huu ndio wakati wa mabadiliko, alisema Othman kwa msisitizo.
Huku hayo yakijiri Othman alikumbusha maumivu ya uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo watu 21 walipoteza maisha Unguja na Pemba, akibainisha kuwa tukio hilo halitasahaulika daima.
Wazanzibari watawaadhibu kwenye sanduku la kura. Msifikiri watu wamesahau madhila ya mwaka 2020, amesema.

Mgombea huyo ameahidi kuwa Serikali atakayoiongoza itahakikisha Zanzibar inapata uhuru wa kiuchumi kwa kudhibiti rasilimali zake bila kikwazo cha Muungano.
Serikali yangu itaondoa utegemezi wa misaada ya nje. Tutajimudu kwa mali zetu za mafuta, gesi na bahari, na kuhakikisha kila Mzanzibari ananufaika moja kwa moja, alisisitiza.
Othman pia aliahidi kuanzisha Mfuko wa Ajira kwa Vijana, kuwezesha ujasiriamali kupitia mikopo nafuu na mafunzo ya kisasa, sambamba na kuzalisha ajira mpya kupitia kilimo, viwanda vidogo, uvuvi wa kisasa na teknolojia.

Ameongeza kuwa wakati wa akina mama wa Micheweni kubanja kokoto kwa mikono yao umepitwa na wakati.
Ameahidi Serikali yake itawekeza kwenye mashine bora na za kisasa ili kuwaondoa wananchi kwenye mateso hayo na kuwapatia heshima na kipato halali chenye staha.
Akizungumzia sekta ya kilimo, amesema Zanzibar itajitegemea kwa chakula kwa kuwekeza kwenye mbegu bora, umwagiliaji na masoko ya ndani na nje.
Tutajenga Zanzibar inayolisha watu wake na kuuza bidhaa nje. Wakulima wetu ndio uti wa mgongo wa uchumi, amesema.
Katika sekta ya elimu, Othman ameahidi mageuzi ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na mazingira ya Zanzibar.
Elimu yetu itawapa vijana ujuzi wa kujiajiri. Tutaimarisha vyuo vya ufundi, teknolojia na bahari, amesema.
Aidha,ameahidi kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali za kisasa kila mkoa, kuhakikisha dawa zinapatikana na kuondoa mfumo wa bima ya afya wenye ufisadi.
Afya ni haki ya kila mmoja. Zanzibar mpya haitakubali tena wananchi kunyanyaswa na huduma mbovu, ameongeza.
Othman amesisitiza kuwa Zanzibar itakuwa kitovu cha uchumi wa buluu, kwa kuwawezesha wavuvi kupata boti za kisasa, vifaa vya kina kirefu na kuwatafutia masoko ya kimataifa.
Amesema pia Serikali yake itaendeleza vivutio vya kihistoria na kitamaduni, kuboresha miundombinu na kuimarisha utalii.
Kila kijiji cha kihistoria kitakuwa kivutio cha utalii na chanzo cha kipato kwa wananchi wake, alisema.
Othman ameahidi kuwekeza kwenye barabara, bandari na viwanja vya ndege, sambamba na kuboresha usafiri wa majini na anga. Pia alisisitiza kuwa ufisadi kwenye miradi yote ya maendeleo utaondolewa kabisa.
Amesema Serikali yake itahakikisha kila kura inalindwa na kila mwananchi anapata uhuru wa kushiriki kisiasa bila hofu.
Hatutakubali tena wizi wa kura. Demokrasia ya kweli ndio msingi wa maendeleo ya Zanzibar mpya, amesema.
Awali, Meneja wa Kampeni wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa, amesema wananchi wa Micheweni wana haki ya kuishi maisha bora kama wenzao duniani.
Cha ajabu leo hata wauza maandazi wanatozwa leseni alisema hii ni kodi ya kumnyonya kila maskini.
Wananchi walioshuhudia mkutano huo walionyesha matumaini mapya.
Amina Suleiman, mkazi wa Micheweni, alisema:
Tumeteseka kwa muda mrefu. Sasa tunaona tumaini jipya kupitia Othman. Tunataka mabadiliko ya kweli.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako