January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman: Maoni ya wananchi yasikilizwe, miswada ya uchaguzi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Leo Januari 3, 2024 Jijini Dar es Salaam, amefungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa Unaoshirikisha Wadau wa Demokrasi ya Vyama Vingi vya Siasa, Kujadili Miswada ya Sheria za Uchaguzi na Mswada wa Sheria za Vyama hivyo.

Katika mkutano huo utakao fanyika kwa muda wa siku mbili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini humo kujadili Miswada iliyowasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba, 10 2023.

Othman amewataka wadau wa masuala ya kidemokrasia, kuitumia nafasi hiyo kujadili kwa weledi ubadilishwaji wa sheria hizo kwa kutumia kanuni za majadiliano ikiwa pamoja na kufuata R4 kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa.

Amesema, ni vyema wadau wakatumia kanuni ya maono mapana ambayo wadau wengi wanayaunga mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akidai kuwa suala hilo si tu kwa ajili ya miswada ya kubadilisha sheria bali ni sehemu ya kutengeneza maono mapana ya Rais ambayo wananchi wengi wanayaunga mkono.

“Ni vyema wadau wakatumia nafasi hii kujadili kwa kutumia kanuni ikiwa pamoja na kanuni ya maono mapana ambayo wengi wanayaunga mkono, leo hii tupo hapa si tu kwa ajili ya miswada ya kurekebisha sheria bali ni sehemu ya kutengeneza maono mapana ya kiongozi wetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo wananchi wengi wanayaunga mkono nayo ni ya ujenzi wa Taifa yaliyojengwa katika R4″ na R Mama iwe ya mageuzi,” amesema Othman.

Aidha, amesema miongoni mwa mageuzi muhimu ambayo nchi inahitaji ni pamoja na kujenga misingi ya uwajibikaji katika ngazi zote, huku akidai kuwa, kulegalega kwa uwajibikaji katika ngazi zote za kiutendaji kwa upande wa kisiasa na Serikali kwa ujumla, hupelekea wananchi kuwa na malalamiko.

Hata Hivyo, Othman ametaka miswada hiyo kuwekwa wazi kwa Umma ili wadau waweze kujadili na kutoa maoni yao, kwa ajili ya kufikia malengo na kutekeleza farsafa ya R4, huku akiwataka wadau hao kuwa jasiri wa kusema na kusikiliza na kufanya mkutano wa amani.

“Hili ni jambo jema sana na linaonesha kumuunga mkono Rais ambaye amekuwa akitoa wito kwamba tuwe tunakutana pamoja kujadili mambo mazito kama hili tulilonalo mbele yetu,” amesema Othman.

Awali akizungumza na hadhara katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, amesema Serikali inategemea kuona maoni yatakayotolewa katika mkutano huo, yanafikishwa sehemu husika bila ‘kuchakachuliwa’ kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Pia amedai kuwa, miswada hiyo baada ya kujadiliwa itawasilishwa tena Bungeni mwezi Februali, mwaka huu.

Hata hivyo, ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa kuandaa mkutano huo wenye lengo la kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka wadau hao kutanguliza uzalendo ili kuwa na mjadala utakao kuwa na tija kwa manufaa ya taifa, huku akisisitiza kuwepo kwa imani kwa kamati itakayoundwa.