November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman: Dhamira njema za Mkapa ziendelee kuenziwa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Hayati Benjamin William Mkapa alibeba azma kubwa ya kujenga mfumo wa uwajibikaji, katika ufanikishaji wa huduma muhimu, kwa maslahi ya Taifa.

Othman ameyasema hayo leo, wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Pili, tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, lililoandaliwa na Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation), katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, kisiwani Unguja.

Amesema kuwa azma hiyo ya Hayati Mkapa, ambayo ililenga kuanzisha na kuendeleza taasisi zenye uwajibikaji kwa kuhusisha kikamilifu Sekta Binafsi, ilikuwa na azma ya kuisogeza Serikali kufanikisha utoaji wa huduma kwa ufanisi, na kwaajili ya maendeleo ya Taifa zima.

Othman amemtaja Hayati Mkapa kuwa maono yake hayo yalipelekea kuongoza juhudi za kuwepo Mipango ya Kuhuisha Uchumi wa Nchi, kupitia Mabadiliko muhimu ya Sera na mazingira bora ya kutekeleza Mfumo wa Ubinafsishaji wa Njia za Maendeleo, ambao ulikwishafikiwa hapo kabla na Watangulizi wake.

Akizindua na kushiriki katika Hatua ya Awali ya Kongamano hilo la Siku Mbili la Kumbukizi iliyobeba Ujumbe wa Mwaka Huu usemao, “Resillient Leadership, Inspiring Change For All”, Othman ameeleza kuwa huu ni wakati muafaka wa kushuhudia na kujadili yale muhimu kutokana na maono ya Hayati Mkapa.

“Pamoja na mambo mengine, utawala wake uliisogeza Nchi mbali, katika kujenga ari ya kujiamini kiuchumi baada ya kuanzisha misingi muhimu ya uwekezaji na uwepo wa taasisi imara zikiwemo za uhamasishaji wa huduma bora za afya kwa jamii, sambamba na kutilia mkazo wa kuhusisha sekta binafsi, matunda ambayo yametuleta hapa leo ili kuyajadili kwa lengo la mafanikio na maendeleo zaidi”, ameongeza Mheshimiwa Othman.

Aidha ametoa wito kwa wajumbe na washiriki wa Kongamano hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania, kuzingatia na kuienzi kwa umakini Dhamira ya Hayati Mkapa kwa Taifa hili, kupitia mijadala yenye upeo, ili hatimaye kuibuka na mbinu zitakazosaidia kuhamasisha maendeleo ya Nchi, wakielewa kwamba yamo mengi ya kujifunza ndani yake.

Katika maelezo yake, kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema kuwa Serikali zote mbili, hapa Visiwani pamoja na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimejifunza mengi kutoka kwa Hayati Benjamin Mkapa, hasa katika uoni wake muhimu wa kuihusisha Sekta Binafsi katika kufanikisha maendeleo ya Nchi.

Mazrui, pamoja na kuishukuru Taasisi ya Mkapa kwa juhudi inazozichukua, amewatoa shaka wahusika wote wa afya serikalini, kwa kusema kuwa Zanzibar kupitia Wizara hiyo imeamua kuitekeleza Sera ya Kujumuisha Sekta Binafsi kikamilifu, kama ulivyokuwa mtazazamo wa Hayati Mkapa, kwa dhamira moja kuu ya kuwafikishia wananchi huduma bora katika jamii, na wala si vinginevyo.

Naye (Kaimu) Waziri wa Afya wa Tanzania Bara, Ummy Mwalimu amemtaja Hayati Rais Mkapa kama Kiongozi ambaye aliisogeza Nchi katika nyanja nyingi za kimaisha wakati wa Utawala wake, zikiwemo maendeleo ya kiuchumi, kijamii na mageuzi ya kisiasa.

Akiwasilisha salamu zake za ufunguzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mkapa, Bi Ellen Mkondya Senkoro, pamoja na kubainisha mafanikio yao makubwa yakiwemo ya ukuzaji wa sekta ya afya, amemuelezea Kiongozi huyo kwa kuwa na upeo wa mbali katika kuimarisha misingi ya uwajibikaji na ufanikishaji wa huduma kwa jamii yote na hata kwa wasiokuwa na sauti.

Mawaziri na Viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali na Jamii, Wanadiplomasia, Wakuu wa Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Wake wa Marais Wastaafu, Mama Anna Mkapa na Mama Shadya Karume – Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Zanzibar, Asasi za Kiraia, Vyama vya Siasa, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zubeir Ali Maulid; na Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Unguja na Pemba, wamehudhuria katika hafla hiyo.