December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman awafariji wagonjwa Zanzibar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, leo tarehe 24 Januari 2023, amefanya ziara maalum ya kuwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa mbali mbali katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Mjini-Magharibi, kisiwani Unguja.

Wagonjwa hao ni Kadhi Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji Khamis; Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), Sheikh Muhidin Zubeir; Amir wa Jumuiya ya Answari Sunna na Naibu Katibu Mtendaji wa JUMAZA, Sheikh Khamis Yussuf; na Mfanyabiashara Mashuhuri hapa Visiwani, Sheikh Ali Abdalla Ali.

Akiwatembelea majumbani kwao kwa nyakati tofauti, huko Magogoni, Saraevo, Magomeni na Chukwani, Othman amewataka wagonjwa hao kuwa na subra kutokana na mitihani ya maradhi, ambapo miongoni mwao wamekuwa wakikabiliana nayo kwa muda mrefu.

Aidha Othman ameeleza kuungana na Viongozi hao Muhimu wa Kijamii, kuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu Awape shifaa, wapone haraka na warudi kuungana na wengine, katika harakati zao za kawaida maishani, na kwaajili ya maendeleo ya Taifa zima.

Akiongea kwa niaba ya wenzake waliotembelewa, Sheikh Khamis Yussuf, ameshukuru hatua ya Kiongozi huyo wa Kitaifa kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa pamoja na watu wasiojiweza, na kumnasihi aendelee na mwenenendo huo muhimu katika ustawi bora wa jamii.

Othman amewajulia hali wagonjwa na watu mbali mbali wasiojiweza hivi karibuni na ambapo pia alifanikisha ziara kama hiyo takriban miezi mitatu iliyopita alipowatembelea wazee na wagonjwa mbali mbali katika Wilaya za Mjini na Magharib Unguja.