October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

OSHA yaongeza maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kwa asilimia 276 ndani ya miaka miwili


Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA)umesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa awamu ya sita  Wakala umefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953 ambapo ongezeko hilo  ni sawa asimilia 276.

Huku  idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia Kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Machi 4,2023 Mtendaji Mkuu wa Wakala huo,Khadija Mwenda kuhusu mafanikio ya wakala katika kusimamia sheria ya usalama wa afya katika miaka miwili ya awamu ya sita amesema kuwa pia kumekuwa na ongezeko la asilimia 175 ya Wafanyakazi waliopata mafunzo ya Usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia Wafanyakazi 43,318. 

Aidha amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320 na  Upimaji afya kutoka Wafanyakazi 363,820 hadi kufikia Wafanyakazi 1,112,237 waliopimwa katika kipindi tajwa.

Mwenda ameeleza kuwa ongozeko hilo lilitokana na kupunguza ada mbalimbali na kuboresha mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa, wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika, ongezeko hili ni tafsiri kwamba hali ya usalama na afya  katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika.

“Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi, maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine105 yalitozwa faini,”amesema.

Akizungumzia mafanikio ya wakala huo Mwenda ametaja Kuimarika kwa shughuli za usimamizi wa usalama na afya mahali pa Kazi, Kupungua kwa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

“Miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kuchunguza ajali mbali mbali zinazotokea katika sehemu za kazi kwa lengo la kubaini vyanzo vya ajali hizo ili kushauri namna bora ya kuzuia ajali kutokea tena hivyo katika kipindi cha miaka miwili, ajali zilizoripotiwa zilipungua kwa asilia 13.2 kutoka ajali 2,138 kupungua hadi kufika 1,855,Magonjwa yanayotokana na kazi yalipungua kwa asilimia 22.1 kutoka wagonjwa 140 kufikia wagonjwa 109,

“Takwimu hizi zinaonesha kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ambayo imepelekea ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kupungua sambamba na kuimarika kwa mifumo hii ya usimamaizi wa usalama na afya, kunapelekea mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa himilivu,”amesema.

Ametaja mafanikio mengine ni pamoja na kupunguza Urasimu na kuboresha   Mifumo ya TEHEMA kwani katika utendaji wa shughuli za wakala Mifumo ya TEHAMA imekuwa ni nyenzo muhimu katika kutoa huduma ambapo mifumo kama TANEPS, GePG, GAMIS, MUSE, E-office imesimikwa na inatumika.