Na Judith Ferdinand,Timesmajira online
Imeelezwa kuwa ongezeko la watu,makazi pamoja na shughuli mbalimbali za kibinadamu kandokando mwa ziwa na fukwe kunachangia kuharibu ikolojia ya ziwa na vyanzo vya maji ambayo itasababisha viumbe hai wa majini kutoweka ikiwemo samaki.
Akizungumza na Timesmajira Online ofisini kwake jijini Mwanza,Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa Jarome Kayombo,ameeleza kuwa uharibufu wa mazingira unaenda sambamba na ongezeko la watu wanaojenga kandokando ya ziwa pamoja na miradi kama hoteli ambao moja kwa moja wanaingiza vitu kwenye ziwa ambavyo siyo vya asili yake.
Ambapo ameeleza kuwa kaya zilizopo maeneo ya kandokando mwa ziwa na fukwe wanazalisha taka maji na ngumu,hivyo endapo wakielekezea ziwani panagekua kuwa dampo hivyo itachangia kugeuza mifumo ya ikolojia ambayo itasababisha kuhama ,kufa kwa viumbe maji pamoja na kuadimika kwa samaki.
Kayombo ameeleza kuwa uharibifu wa mazingira unaenda sambamba na ongezeko la watu kwa sababu kinachoathiri mazingira ni shughuli za wanadamu hivyo kama watu watajenga na kufanya shughuli ndani ya mita 60 maana yake watabadilisha mfumo wa kiikolojia ya ziwa.
“Kwa sababu kunapokuwa na ongezeko la watu katika fukwe zetu na wamejenga mpaka mita ziro yani hadi zile ndani ya mita 60 hawajaziheshimu, maana yake ni nini hizi kaya zinazalisha taka maji na ngumu hivyo vyote vikitupwa kwenye ziwa linageuka kuwa dampo,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Mfano mimi nikizalisha maji yangu machafu ya chooni naelekeza ziwani nimefagia nimezalisha takataka ziwani,kwaio kila kitu kitaenda kule kwa maana ya ziwa lina kazi yake ya kutunza viumbe hai kama samaki na viumbe wengine sasa linapokuwa dampo mfumo wa ikolojia unabadilika na samaki watapungua na viumbe maji kutoweka kabisa kwa sababu tumeingiza kitu ambacho kwa asili siyo sehemu yake,”ameeleza Kayombo.
Sababu ya Sheria ya mazingira kukataza shughuli ndani ya mita 60
Ujenzi kwenye fukwe sheria ya mazingira imesema kuwa hakuna shughuli inayoruhusiwa toka maji yanapoishia hadi mita 60 ambapo mita hizo kubaki siyo kuwa hazina maana hapana sababu wanaamini mifumo ya ikolojia ya ziwa inategemea uoto au viumbe wanaopatikana kandokando ya ziwa.
“Ndio maana tunasema sheria imekataza shughuli kufanyika ndani ya mita 60, lakini ukiangalia hasa kwenye miji mikubwa na hata vijijini kuna shughuli zinafanyika ndani ya mita 60 ikiwemo kilimo kinyume na sheria,” ameeleza Kayombo.
Kayombo ameeleza sababu ya sheria ya mazingira kukataza shughuli yoyote ikiwemo ya ujenzi kufanyika ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji kama ziwa,bahari ni pamoja na mifumo ya ikolojia ya majini na nchi kavu kutegemeana.
Ambao ametolea mfano kuwa kama unalima ndani ya mita 60, kwanza utaondoa uoto wa asili wote ambao upo katika eneo hilo ambao unaweza kusababisha mmomonyoko wa udogo
pia umeondoa madharia ya viumbe hai na maana yake hao viumbe watatoweka na pia itaharibu mfumo wa kiikolojia kwa viumbe hai wanaoishi ziwani.
Ameeleza kuwa ukiondo uoto wa asili na kuweka miradi mingine maana yake zile taka zinaingia moja kwa moja ziwani ambapo kuna madharia ya viumbe hai ambao pengine wanaishi kwenye nchi kavu na majini mfano mamba hakai ziwani pekee yake kuna muda anakuwa nchi kavu kenge pia pamoja na viumbe wengine kama hao.
“Ule uoto uliopo pembezoni mwa ziwa,mto au bahari vinauhusiano wa moja kwa moja na viumbe hai vilivyopo majini au ziwani, usipo kuwepo ndani ya mita 60 kwa mfano tuchukulie suala zima la mmomonyoko wa udogo ule uoto unasaidia kushika udongo au takataka zitokazo nchi kavu zisiingie moja kwa moja ziwani ikiwemo mifuko ya plastiki,”ameeleza Kayombo na kuongeza kuwa
“Kama kukiwa hakuna uoto takataka zitenda moja kwa moja ziwani lakini kama hapa katikati mita 60 zimeachwa na kuna uoto maana yake itakuwa kama chujio la kuchuja baadhi ya takataka zisiingie moja kwa moja ziwani na kusababisha uchafuzi wa ziwa”.
Sababu ya baadhi ya miradi na shughuli kufanyika ndani ya mita 60
Kayombo amefafanua kuwa kuna vitu viwili ambavyo vinaweza kuchangia shughuli au miradi kufanyika ndani ya mita 60, kandokando,fukwe au ndani ya maji ameeleza kuwa kwanza kuna miradi ili iweze kujengwa lazima ijengwe ndani au karibu na eneo la ziwa.
Ni miradi ambayo inauhusiano wa moja kwa moja na ziwa au mto na vitu kama hivyo kwa mfano unajenga gati kwa ajili ya meli huwezi ukajenga nje ya mita 60 kwa sababu meli inatembea majini huwezi kusema itoke nje ya mita 60.
“Kitu cha msingi ni lazima wafanye tathimini ya athari ya mazingira ambao ni mchakato pekee kwa nchi yetu ambayo unaweza kuainisha athari zinazotokana na mradi husika na kuanza kutengeneza sasa mkakati wa kupunguza au kuondoa athari wakati mradi unapokuwa ukifanya kazi,”ameeleza Kayombo.
Pia ameeleza kuwa kuna miradi ilijengwa kabla ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 haijatungwa ambapo walijenga majengo ndani ya mita 60 ambao sasa hao wanafanya ukaguzi wa mazingira ambao wanaainisha athari gani wanaweza kuwa wanasababisha katika mradi wao nao wanatengeneza mpango mkakati kwa ajili ya kuondoa athari hizo.
“Sheria haisemi uendelezaji ni sifuri (zero development),lakini kuna mchakato ambao wataalamu watajiridhisha kuwa mradi wako hautasababisha athari kubwa za mazingira na kutambua athari zinazoweza kujitokeza na mfumo gani uwekwe kupunguza ama kumaliza athari hizo,”.
Jitihada za Nemc katika kukabiliana na changamoto hiyo
Kayombo ameeleza kuwa Nemc imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuhimiza kabla mtu ajaanza ujenzi au kufanya mradi wowote kufanya tathimini ya athari za mazingira ili kujiridhisha mradi wake utasababisha athari zipi na kitu gani kitafanyika kupunguza athari hizo.
“Mfano tuna viwanda vya samaki,hoteli hao wote tunawataka kufanya tathimini ya mazingira kujua watazalisha taka kiasi gani,taka maji kiasi gani na taka ngumu pia kiasi gani na hatuambie anatupa wapi akituambia anatupa ziwani tunamwambia hapana ila tunataka aweke miundombinu ya kuhakikisha taka zake haziingii ziwani kama ni viwanda vya samaki na vingine tunamtaka asitupe maji taka ziwani kabla maji hayo hayajatibiwa kwa viwango vinavyotakiwa ili kurudishwa ziwani,”ameeleza.
Pia wanatoa elimu kwa wanaoishi kandokando ya ziwa ili kupunguza athari za uchafuzi wa ziwa Victoria na tatu kwa wale wenye shingo ngumu sheria inachukua mkondo wake ambapo wameisha adhibu viwanda,hoteli na mwananchi mmoja mmoja ambao wamekiuka taratibu za kisheria.
Hivyo ametoa wito kwa wadau wote kuzingatia sheria,taratibu na kanuni za mazingira ili kuepuka athari za uchafuzi wa mazingira kimsingi nemc hawapendelei kutoa adhabu kwani siyo kipaumbele chao mtu afanye kosa wampe adhabu bali kipaumbele ni mtu aelewe na asifanye kosa.
“Eneo la fukwe siyo Nemc pekee ndio tunalisimamia mfumo wa ikolojia ya ziwa na fukwe hailindwi na nemc pekee ila tunawenzetu wa bonde la Ziwa Victoria,Wizara ya uvuvi kwa sababu wanategemea Ziwa kupata samaki ambao wanategemea sana fukwe na Ziwa lenyewe lipo katika hali gani, Halmashauri wanasimamia.
BMU kwa ajili ya kulinda fukwe pamoja na Mwananchi mmoja mmoja ambao wamekuwa wakiondoa uoto na kutupa taka moja kwa moja ziwani hivyo kuharibu ikolojia ya Ziwa na fukwe.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Mhandisi Gerald Itimbula,anaeleza kuwa katika kudhibiti ujenzi na makazi ya watu wanaoishi pembezoni mwa ziwa Victoria,sekta mbalimbali ziwe na sauti moja.
“Hakuna sheria inayoruhusu makazi pembezoni mwa ziwa ama ndani ya mita 60 hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha rasilimali ya maji inatunzwa maana ni fahari yetu na vizazi vijavyo,”.
Mhandisi Gerald anasema mkanganyiko wa kisekta kwenye hatua za kuchukua kwa waliokiuka sheria na kujenga ndani ya mita 60 ni tatizo hivyo wanaohusika kutoa vibali ni wakati wa kukubaliana na kuwa wamoja.
Anaeleza kuwa palipo na makazi kuna uzalishaji wa taka aina zote ambao unachangia uchafuzi wa ziwa na kuathiri uhalisia na uoto wa asili hivyo katika kupambana na suala hilo hatua mbalimbali wamezichukua ili kuhakikisha uchafuzi wa mazingira haufanyiki ikiwemo kuwapa baadhi ya watu notice sambamba na kuwachukulia hatua mbalimbali.
” Kuanzia January hadi sasa watu wengi tumewachukulia hatua wapo ambao walipewa barua za nia yetu ya kuwashitaki kwa sababu ya kukiuka sheria tulitoa nia ya kuwapeleka mahakamani wapo ambao ilibidi wasitishe shughuli zao mpaka wafanye wanayotakiwa pia kuna kampuni ambazo tutazichukulia hatua,” anaeleza Gerald.
Aidha anaeleza kuwa bado wanahitaji kuwa na vikao vya ndani vya namna ya kuboresha utaratibu wa watu wanaojenga karibu na ziwa huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi ili watambue athari wanazoweza kuzipata wanapojenga katika maeneo hayo na waweze kuondoka miundombinu yao wasipate madhara.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Butuja uliopo kandokando mwa Ziwa Victoria wilayani Ilemela mkoani Mwanza Kichonge Mwita anasema kuwa miundombinu katika eneo lake ni tatizo kwa sababu wananchi wengi wanaoishi katika mtaa huo ni wavuvi na wanaishi pembezoni mwa ziwa.
Hivyo ufinyu wa mitalo kunachangia kutopitisha maji na kuleta mafuriko hasa vipindi vya mvua hivyo wanaiomba serikali kuwaboreshea miundombinu hiyo ili kuondokana na uchafuzi wa mazingira.
“Siku moja mvua ilinyesha sana,maeneo yetu yalijaa maji watu hawakutoka kwenda kwenye shughuli zao, wanafunzi nao hawakwenda shule mimi nilikuwa na mbuzi wangu amezaa ilisombwa na maji pamoja na mtoto wake,pia ndani ya nyumba zetu kulijaa maji yaani maeneo haya kipindi cha mvua ni hatari sana,” anaeleza Mwita.
Pia anasema kuwa changamoto inayowakumba kuwa tatizo lingine linalowakumba ni milipuko ya magonjwa kutokana na wigi wa watu wanaoishi maeneo hayo kutokuwa na vyoo hivyo wanaiomba serikali kuwaboreshea miundombinu ya maji,umeme ,barabara ili wananchi wake waweze kunufaika na kuendelea kulijenga taifa.
Mmoja wa wakazi wa mtaa na Mwalo wa Butuja ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, anaeleza kuwa chanzo cha wananchi kukimbilia maeneo ya mialo na kandokando mwa ziwa kuweka makazi na kufanya shughuli mbalimbali ni kutokana na bei ya viwanja pamoja na gharama za maisha kuwa chini.
Licha ya unafuu huo lakini wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko yanayochangiwana uchafuzi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo hayo kujisaidia hovyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo pembezoni mwa ziwa kwa sababu hawana vyoo.
Pia athari nyingine wanazokumbana nazo nyakati za mvua ni kubwa ikiwemo nyumba zao kuharibika,kubomoka pamoja na kupoteza vitu vyao vya thamani kutokana na maji kujaa baada ya maji kuongezeka ziwani.
” Watu wanakwepa maeneo mengine Kwa sababu ya gharama maeneo haya mara nyingi ni ya gharama za chini kuna viwanja kuanzia elfu 50
ukitaka kujenga unajenga kwa kiasi kidogo cha fedha lakini kweli mazingira siyo rafiki yote haya ni uduni wa maisha “anaeleza.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia