Na Victor Nakinda, TimesMajira Online
TANZANIA ni nchi iliyojaaliwa ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kustawisha mazao mbali mbali ya chakula na biashara. Maeneo mengi nchini Tanzania yana mito, mabwawa na vyanzo vingine vya maji huku yakipata wastani mzuri wa mvua hali inayochagiza kilimo na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula na biashara.
Ikiwa hali ni hiyo kama Taifa hatuna sababu ya kuhangaika kuagiza bidhaa iwe ni ghafi au za viwandani zinazotokana na mazao ya kilimo kwa kuwa tunazo rasilimali zote muhimu kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Sanjari na ardhi kubwa yenye rutuba inayostawisha mazao ya aina nyingi, Tanzania tuna idadi kubwa ya watu na siasa safi ambayo inawapa uhuru watu wake kuzalisha mali pasipo tishio la usalama huku watu hao wakiwa huru kwenda popote nchini kufanya shughuli halali za kiuchumi ikiwemo kilimo.
Pamoja na hali hiyo inaelezwa kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa mafuta ya kupikia kiasi cha tani 365,000 huku mahitaji halisi yakiwa ni wastani wa tani 570,000 kwa mwaka ambapo uwezo wa uzalishaji wa ndani wa bidhaa hiyo muhimu ni tani 205,000 tu na hivyo kulazimu kuagiza kiasi cha tani 365,000 kutoka nje ya nchi.
Kiasi cha mafuta ya kupikia tunachoagiza nje ya nchi kinaligharimu taifa zaidi Shilingi Bilioni 443 ambazo zinatumika kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi. Fedha ni nyingi ambazo kama tungelikuwa tunajitosheleza katika uzalishaji wa mafuta hapa nchini, kiasi hicho kingeliokolewa na kuelekezwa maeneo mengine kama vile uboresha na utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu.
Uhaba wa mafuta ya kupikia hauikabili tu Tanzania bali pia nchi za Afrika ya Mashariki ambazo kwa pamoja uagizaji wake wa mafuta nje ya nchi hizo ni asilimia 48 mpaka 85 kwani hazizalishi mafuta kwa wingi kwa kiwango cha kujitosheleza mahitaji yao ya ndani hali inayowapelekea pia kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi hizo.
Nchi za ukanda wa SADC ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya kupikia ambapo huagiza aslimia 60 wa bidhaa hiyo muhimu.
Kwa muktadha huo tunaona kuwa endapo tutaelekeza nguvu zetu kama Taifa, katika uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta, kwanza tutajitosheleza kwa kupata mafuta ya kupikia ndani ya nchi lakini pia tutakuwa na uhakika wa soko la mafuta kwa kuuza mafuta hayo kwa majirani zetu wa Afrika Mashariki, nchi zilizo katika ukanda wa SADC na nchi nyingine Duniani hivyo kukuza pato ta Taifa.
Frank Reuben ni Mtafiti wa Mbegu za Mafuta kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kilichopo Ilonga, Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro. Akizungumza na mwandishi wa makala hii Frank,ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa zao la alizeti alisema kuwa ipo mipango ya muda mfupi wa kati na ya muda mrefu ya kupambana na uhaba wa mafuta ya kupikia nchini kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta.
Frank anayataja mazao ya mbegu za mafuta kuwa ni alizeti, karanga, minazi, michikichi na pamba. Anasema kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa Taifa linaongeza uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ili kujitosheleza nchini na hata kuuza nje ya nchi.
Frank anasema kuwa pamoja na mazao mengine yanayozalisha mbegu za mafuta, Serikali imeweka mkazo katika uzalishaji wa zao la Alizeti na Michikichi kwa kuhakikisha kuwa mazao hayo yanafanyiwa utafiti wa kina, kuzalishwa kwa wingi kwa mbegu na miche na kusambazwa kwa wakulima mahali pote nchini ili waweze kulima kwa wingi kwa lengo la kuzalisha mafuta kuelekea kujitosheleza kwa bidhaa hiyo kwa soko la ndani na hatimae soko la nje.
ZAO LA ALIZETI
Frank anasema kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa Alizeti barani Afrika na ni nchi ya kumi kwa uzalishaji wa Alizeti Duniani huku akilitaja zao hilo kuwa linastawi maeneo yote hapa nchini.
“Nchini Tanzania zao la alizeti linaweza kulimwa maeneo yote nchini. Zao hili linachangia asilimia 70 ya uzalishaji wa mafuta ambazo ni tani 143,500,kati ya tani 205000. Zao hili linahitaji kulimwa eneo kubwa kwa lengo la kuzalisha tani nyingi za mbegu na hatimae mafuta.
Anasema kuwa kituo cha utafiti TARI Ilonga, kimepewa dhamana ya kufanya utafiti na kuratibu utafiti wa kitaifa wa zao la Alizeti ikiwa ni mpango wa muda mfupi wa kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, huku yeye akiwa amepewa dhamana ya Uratibu wa zao hilo kitaifa.
“Kwa upande wa zao la alizeti tunazo mbegu za madaraja mbali mbali kama vile mbegu za awali, mbegu za msingi, na mbegu zilizothibitishwa ubora.
Mbegu zilizothibitishwa ubora zimefanyiwa utafiti wa kitaalamu ambapo tunazalisha na kuwapa mashirika mbali mbali yanayosambaza mbegu kwa lengo la kuzisambaza kwa wakulima ambao ni wadau muhimu ili waweze kuzalisha malighafi za kupeleka kwenye viwanda vya kukamua mafuta.” Anaeleza Frank.
Frank anaongeza kusema kuwa lengo kubwa la kufanya utafiti ni kuunga mkono sera za Serikali ambazo zimetaja kuweka nguvu na msukumo mkubwa katika kufanya utafiti wa mazao ya mbegu za mafuta sambamba na kuongeza uzalishaji wake.
“Uzalishaji wa sasa wa zao la alizeti hapa nchini ni tani 790,000 ambapo sera ya Serikali imeweka lengo la kuzalisha tani Milioni 1.5,mpaka kufikia mwaka 2025. Sisi TARI kwa kushirikiana na wadau wengine wa uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta tumejiwekea lengo la kufikisha tani Milioni 2 ili kuweza kupata mafuta tani 700,000 kufikia mwaka 2025. Kiasi hicho cha mafuta ya tani 700,000 kinakadiriwa kuwa hitaji ifikapo 2030.
Frank anasema kuwa licha ya kufanya tafiti za mbegu bora za alizeti, kituo cha TARI Ilonga,kinauza mbegu za zao hilo ambazo ni za daraja lililothibitishwa ubora (daraja la kibiashara) kwa shilingi 4,000 kwa kilo moja bei ambayo ipo chini ya bei ya mbegu hizo katika maduka ya pembejeo za kilimo na maeneo mengine yanayouza mbegu hizo ambapo huuzwa kwa Shilingi 35,000 kwa kilogramu moja.
Anasema kuwa lengo la kuuza bei rahisi mbegu hizo ni kushawishi idadi kubwa ya wakulima kumudu gharama ili waweze kuzalisha kwa wingi zao hilo muhimu kwa ajili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia nchini.
Frank anayataja mafuta ya alizeti kuwa ni mafuta bora kwa afya ya binadamu kwa kuwa hayana rehemu, hivyo anasisitiza wakulima kote nchini kuweka nguvu katika kuzalisha zao la alizeti ili kujitosheleza mahitaji ya mafuta ya kupikia sambamba na kutunza afya zao kwa kutumia mafuta ya alizeti.
“Mimi kama Mratibu wa Kitaifa wa zao hili la alizeti, ninashirikiana kikamilifu na wataalamu wenzangu kuhakikisha tunatatua changamoto zote za kitaalamu juu ya zao hili na mazao mengine ya mbegu za mafuta ili tuweze kwenda na kasi ya wakulima kwa kuzalisha mbegu bora na kwa wingi ili tukutane na mahitaji kwa lengo la kuleta tija inayokusudiwa katika Taifa letu” anasema Frank.
Frank anashauri wakulima pindi wanapolima zao hilo watundike mizinga ya nyuki kwenye mashamba yao kwa kuwa nyuki wana umuhimu mkubwa katika uchavushaji wa zao hilo na kufanya mbegu zikomae vizuri na kuleta mavuno bora.
ZAO LA MICHIKICHI
Kilimo cha zao la michikichi, ni mkakati wa Serikali kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kupikia nchini ni kuhamasisha ulimaji wa zao la michikichiki, zao linalotajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha kwa wingi mafuta ya kupikia.
Frank Ruben, mtafiti wa mazao ya mbegu za mafuta, kituo cha utafiti TARI Ilonga, anasema kuwa zao la michikichi huzalisha mafuta mara tano zaidi kulinganisha na mazao mengine ya mbegu za mafuta. Anasema kuwa mche mmoja wa mchikichi hutoa lita 28 mpaka 38 ambazo ni sawa na tani tano kwa hekta. Pamoja na mafuta ya kula yanayoitwa mawese pia hutoa mafuta ya mise yanayotumika kutengeneza sabuni.
Frank anaongeza kusema kuwa hekta moja ya zao la michikichi aina ya chotara inazalisha tani tano za mafuta hivyo anatoa wito kwa wakulima kote nchini kujikita katika kilimo cha michikichi, kilimo chenye tija kubwa.
“Pamoja na mambo mengine TARI Ilonga kwa kushirikiana na kituo cha TARI Kihinga kilichopo mkoani Kigoma, tunazalisha miche ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima wa mikoa ya kanda ya Mashariki ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga.”
Frank anasema kuwa kwa kuzingatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasimu Majaliwa, kuhusu kuongeza kasi ya kilimo cha zao la michikichi kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini TARI Ilonga wamezalisha miche 80,000.
“ Tunatii na kutekeleza agizo la Serikali la kuongeza uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta. TARI Ilonga, tumezalisha miche 80,000 ya mbegu bora za michikichi na tayari tumeanza kuigawa bure kwa wakulima wa mkoani Morogoro na wa mikoa jirani. Tunaamini kuwa hatua hii itawaongezea ari na mori wakulima kujikita katika kilimo cha zao hili linalozalisha mafuta kwa wingi.” Anasema Frank.
Frank anaongeza kusema kuwa miche ya michikichi wanayoigawa bure kituoni hapo imefanyiwa utafiti wa kutosha, inastawi vizuri, inakabiliana na magonjwa na inatoa mafuta kwa wingi na hivyo anawaasa wakulima kutohofia kulima zao hilo huku akieleza kuwa ndani ya shamba la michikichi unaweza kupanda mazao mengine ya muda mfupi ya mbegu za mafuta kama vile alizeti na ufuta.
WITO
Frank anatoa wito kwa mkulima mmoja mmoja, taasisi za Serikali, taasisi binafsi na mashirika mbali mbali yanayojishughulisha na kilimo, kuunga mkono sera ya Serikali ya kupambana na kumaliza uhaba wa mafuta ya kupikia nchini, kwa kujikita katika uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta kwa kulima mashamba makubwa huku wakifuata kanuni kilimo bora ambazo zitapelekea mavuno kwa wingi na kumaliza uhaba wa mafuta nchini.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia