April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ombi kwa serikali kuanza kutoa elimu ya chanjo ya uviko-19 shuleni

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Tangu serikali ilipoanza kutoa chanjo ya uviko-19,imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.

Licha na jitihada hizo baadhi ya wanafunzi katika shule za sekondari zilizopo jijini Mwanza wameeleza kuwa katika mazingira yao ya shule bado elimu hiyo haijawafikia.

Hivyo wameomba kupatiwa elimu ya chanjo ya uviko-19 ili waweze kuwa na uelewa juu ya chanjo hiyo na kuweza kuhamasisha jamii na wazazi wao kupata chanjo hiyo.

Akizungumza na timesmajira jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya kupokea Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Nyamagana pamoja elimu ya sensa ya watu na makazi, uliofanyika uwanja wa Nyamagana,mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameeleza kuwa licha ya kuwa chanjo ya uviko-19 inatolewa kwa watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.

Lakini ni vyema elimu kuhusu chanjo hiyo ikatolewa hadi kwa wanafunzi shuleni ili wawe na uelewa na kufahamu umuhimu wa chanjo katika kupambana na ugonjwa wa corona na magonjwa mengine.

“Hii itasaidia hata tutakapo fikisha umri wa miaka 18 iwe rahisi kukubali kupata chanjo hiyo na chanjo nyingine ambazo serikali imekuwa ikihamasisha kwani nitakuwa ninauelewa tayari tangu muda mrefu wa nini faida za kupata chanjo katika kupambana na magonjwa,”ameeleza.

Kwa upande wake Nyamwiza Lucas, ameeleza kuwa wakiwa na elimu na uelewa juu ya chanjo hiyo wataendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wazazi na jamii ili iendelee kupata chanjo hiyo.

Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Agoustine Tanzania (SAUT) kwa Mkoa wa Mwanza Evarist Mapesa,ameeleza kuwa kwa upande wa chuo hicho serikali imekuwa ikitoa elimu kuhusu chanjo ya uviko-19 kupitia makongamano chuoni hapo.

“Chuoni kwetu kumekuwa na makongamano na kupitia makongamano hayo uongozi wa chuo na Wizara ya Afya wamekuwa wakija na kutupa elimu ya corona na umuhimu wa chanjo ya uviko-19,ili kuondoa imani potofu dhidi ya chanjo hiyo ilijengeka kwa jamii,”ameeleza Mapesa.

Naye Mwalimu wa Shule ya Sekondari Pamba Edwin Ngonyani, ameiomba serikali kutoa elimu ya uviko-19 kwa wanafunzi na watoto kwa ajili ya kuipeleke kwa wazazi ambao wakielimishwa watakubali kupata chanjo hiyo.

“Sisi shule ya sekondari Pamba tunayofuraha kwamba serikali kupitia vyombo vyake walifika shuleni na kutupa elimu bora ya chanjo ya uviko-19,na waliongea na wanafunzi na kuweka programu ya walimu kuchanja ambao waliitikia muitikio na watu walichanja,”ameeleza Mwalimu Ngonyani.

Baadhi ya wanafunzi jijini Mwanza wakiwa katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo uadhimisha kila ifikapo Juni 16 ambapo kimkoa yamefanyika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza.( Picha na Judith Ferdinand)