November 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi za CAF zazinduliwa rasmi Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

TANZANIA, imeandika historia barani Afrika baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kukabidhiwa rasmi ofisi za shirikisho hilo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, itakayofanyika hapa nchini.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameungana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Samson Adamu kutoka Nigeria, pamoja na viongozi wengine kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Ofisi za CAF jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huo ulifanyika leo, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo ofisi hizo zitakuwa kitovu cha shughuli za Sekretarieti na uratibu wa maandalizi ya Fainali za AFCON 2027, zilizohamishiwa Dar es Salaam kutoka Nairobi,

Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 itakuwa fursa ya kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa na kukuza biashara nchini, huku akiwataka Watanzania kujiandaa kunufaika na ujio wa wageni.

Makonda amesema Tanzania inatarajia kupokea wageni kati ya 500,000 na 700,000, huku zaidi ya watu bilioni tatu duniani wakitarajiwa kufuatilia michuano hiyo.

Amesema, Serikali inajipanga kuhakikisha wageni watakaofika nchini wanapata huduma bora, wanakaribishwa na wanarejea salama katika nchi zao.

Hata hivyo, amewataka Watanzania kuonesha ukarimu na kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na ongezeko la wageni na mzunguko wa fedha.

Pia, amesema michuano hiyo ni nafasi ya kuitangaza Kiswahili, akikitaja kuwa tunu ya taifa inayoweza kupata mwonekano mkubwa zaidi kimataifa kupitia mashindano hayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Serikali imeamua kutumia michezo kama nyenzo ya kukuza utalii, kuongeza shughuli za kiuchumi na kupanua mnyororo wa thamani katika biashara mbalimbali.

Amesema AFCON 2027 itaiwezesha Tanzania kujitangaza kimataifa katika sekta za michezo na utalii, huku Serikali ikishirikiana na wadau kuhakikisha maandalizi yanazingatia mahitaji ya usalama, afya, biashara na miundombinu.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), Leodger Tenga, alisema Tanzania iko tayari kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza rasmi Juni 19, hadi Julai 17, 2027, kwa kushirikisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

“Ni fahari na heshina kubwa kwetu kwa Tanzania kupata nafasi hii muhimu, nikiri wazi tumejiandaa vizuri na tupo tayari kuonyesha kwa vitendo namna nchi yetu ilivyodhamiria kuleta mageuzi makubwa,” amesema Tenga.