December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaokoa trilioni 11.4/-

Na Joyce Kasiki,TimesMajira, Online Dodoma

OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuokoa sh.Trilioi 11.4 za Serikali baada ya kushinda kesi za nje na ndani ya nchi zilizokuwa zikiikabili Serikali.

Aidha ofisi hiyo imefanikiwa kuokoa mashamba 106, hotel na nyumba ambazo zilitaifishwa kinyume na sheria.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata ameyasema hayo jijini hapa jana wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika utendaji kazi wao.

Wakili huyo amesema mali za Serikali zilizookolewa ni pamoja na kesi ya ndege iliyokamatwa Afrika Kusini na Canada ambazo walipambana kuhakikisha wanashinda na kuokoa kiasi cha fedha kilichojumuisha na kesi nyingine.

Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata akifungua mafunzo ya kuwanoa mawakili nchini.

“Kuna kesi nyingi ambazo tumezisimamia na kushinda jambo ambalo limepelekea kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, tusingeshinda ina maana ingetugharimu,”amesema Wakili Mkuu wa Serikali Malata.

Amesema kutokana na hilo imeonesha jinsi gani kitengo hicho kilivyo muhimu kwa taifa kutokana na kusimamia sheria pale wanapostahili kufanya hivyo.

“Tumeokoa pia mashamba,nyumba,viwanja na mali nyingine za Serikali lengo ni kuona haki inatendeka katika mali za Serikali,”amesisitiza
Amebainisha kuwa mashamba waliyaokoa ni 106, Mbeya Hoteli na viwanja ambavyo vimerejeshwa katika Shirika la Reli na nyumba ambazo nazo zimerejeshwa kwa wahusika.

Wakili Mkuu huyo amesema kutokana na kazi hizo muhimu ambazo wanafanya, mawakaili ndio maana wameandaliwa semina hiyo ya siku tatu ambayo wanaamini itawajengea uwezo mkubwa zaidi katika utendaji kazi wao.

Amesema baadhi ya mambo ambayo watajifunza katika semina hiyo ni ujuzi stadi katika maeneo mbalimbali yanayowahusu.

Pia amesema mawakili hao watajengewa uwezo kusimamia hati za madai,kuendesha mashtaka ya ushahidi,wajibu wa Wakili wa Serikali,pamoja na miiko na maadili katika kazi ya uwakili.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju ameipongeza ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutokana na kuandaa Semina hiyo ambayo wanaamini italeta manufaa makubwa kwa mawakili kwa kuwa watapata muda wa kujifunza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju akizungumza katika semina hiyo.

Ametaka mawakili wanaopewa mafunzo hayo kuhoji kwa wakufunzi pale ambapo hawajaelewa ili wakitoka wawe wameiva katika uwakili wao.

“Mawakili wanajua kazi yao lakini semina hii itawasaidia zaidi kuongeza ujuzi, “amesema Mpanju.

Mpanju amesema waitumie semina hiyo kujifunza na kuongeza taaluma ili watakapoingia ofisini kwa ajili ya kusimamia sheria wafanye kazi hiyo kwa usahihi.