Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline Dodoma
WIZARA ya Katiba na Sheria imesema ipo haja ya kuimarishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kusaidia kusimamia mashauri yote yanayoikabili Serikali ya ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jijini hapa na Waziri wa wizara hiyo, Prof.Palamagamba Kabudi wakati alipokuwa anatoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambapo amesema kuwa hali hiyo itasaidia kuiondolea mzigo wa gharama kubwa ya fedha Serikali ambayo imekuwa ikitumia kwa ajili ya kulipa mawakili wa nje ya nchi.
Amesema kuwa, ipo haja kwa Serikali kuendelea kuboresha utendaji kazi wa ofisi hiyo ili kusadia kusimamia kesi zote za serikali za ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa, hali hiyo itasaidia taifa kuondokana na matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kulipa mawakili wa nje pale Taifa linapofunguliwa kesi nje ya nchi.
“Hawa viongozi wetu Mama Samia hata wakati ule wa Hayati Magufuli wanapata shida sana unakuta wametenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye miundombinu au miradi ya maendeleo lakini unakuta nchi inashitakiwa na kwenda mahakamani unatakiwa kutumia fedha nyingi sana kulipa mawakili,”amesema Prof. Kabudi.
Pia amesema kuwa kesi ambazo zimekuwa zikifunguliwa zinailazimu nchi kulipa mamilioni ya fedha ambayo yangetumika katika miradi mingine ya maendeleo.
“Hivi sasa tuendelea tuu na hiki kipindi cha mpito lakini baadaye nataka ofisi hii ndiyo iwe inasimamia kesi zote za serikali za ndani na nje tutafanikiwa tuu kama tutaendelea kuimarisha Ofisi hii ya Wakali mkuu wa serikali,”amesema.
Hata hivyo amewataka mawakili wa mashirika ya umma ambao wamekuwa wakisimamia kesi mbalimbali kutoa taarifa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na siyo kusubiri hadi hali inapokuwa mbaya.
“Mawakili wote wa mashirika ya umma lazima wawajibike kwa Wakili mkuu wa serikali na kesi zote lazima waripoti kwa Wakili mkuu siyo kusubiri hadi mambo yanakuwa magumu ndiyo wanaripoti,”amesema.
Prof. Kabudi amesema, ipo haja ya kuwa na taasisi ya mafunzo ya Mawakili wa Ofisi ya Serikali ambayo itatumika kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha utendaji kazi wao.
Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, amesema kuwa pamoja na mafanikio waliyoyapa ikiwemo kuokoa fedha za serikali lakini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo idadi ndogo ya watumishi.
Malata,ametaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari katika ofisi zao 16, ambazo hadi sasa zina magari 15.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa