May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahamasishwa kutumia bidhaa za ngozi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WITO umetolewa kwa watanzania nchini kutumia bidhaa za ngozi ambazo zimekuwa zikizalishwa na Viwanda vya ndani ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya kuwa na uchumi imara unaotegemea Viwanda.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa leseni kwa wachunaji wa ngozi kutoka Manispaa ya kinondoni, Temeke na Ilala, Ofisa Biashara Mkoa wa Dar es salaam, Thabit Massa amesema kwa sasa bidhaa ya ngozi imekuwa ikizalishwa kwa viwango vikubwa kutokana na kuwepo kwa Viwanda na uwekezaji mkubwa.

Amesema, katika mwaka 2019/20 jumla ya vipande vya ngozi millioni 11.77 vinakadiliwa kuzalishwa huku Uzalishaji wa ngozi ukiwa sawa na uvunaji wa asilimia 12.5 kwa ng’ombe, asilimia 28.0 kwa mbuzi na asilimia 29.0 kwa kondoo.

“Wastani wa Uzalishaji wa ngozi kwa siku ni vipande 31,000 ambapo vinauwezo wa kuzalisha futi za mraba millioni 138.57 kwa mwaka zenye uwezo jozi viatu 55.42,”amesema Massa.

Massa amesema,tasnia ya ngozi kwa sasa imekuwa ambapo kwa sasa kuna Viwanda vitano vinavyosindika ngozi kati ya hivyo vinavyosindika ngozi kufikia hatua ya mwisho.

Akitaja viwanda hivyo ni pamoja kiwanda cha ACE Leather cha mkoano Morogoro, Leather Industry Ltd Moshi, Himo Tannery and Planters Ltd ambapo vinauwezo wa kusindika futi mraba 110,000,15000 na 10,000 kwa siku.

Baadhi ya wachunaji wa ngozi kutoka katika machinjio mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kupokea leseni za uchunaji ngozi kutoka kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Hata hivyo amesema, katika kutambua hilo wizara imefanya tathimini ya ubora wa ngozi katika machinjio yenye wachunaji kwa kutoa mafunzo na kuwapatia leseni.

“Tumefanikiwa kuendesha mafunzo ya wachunaji wa ngozi 432 wa machinjio ya manispaa za Jiji la Dar es salaam mwezi Januari ambapo leo tunawapatia leseni,”amesema.

Na kuongeza kuwa Wizara imewajengea uwezo wakaguzi na waweka madaraja ya ngozi wa mkoa wa Dar es salaam, Pwani na Morogoro.

Aidha, aliwataka wachunaji kuzingatia mbinu mpya za uchunaji bora za ngozi huku alisisitiza kuwa wasimamizi wa machinjio kuanzia sasa kutoruhusu mtu asiye na leseni kuingia katika machinjio.

Awali Kaimu Mkurungezi Uzalishaji Mifugo na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Gabriel Bura amesema lengo la kutoa mafunzo na leseni kwa wachunaji ni kuhakikisha bidhaa ya ngozi inaweza kuzalishwa katika Viwanda vikubwa.

Amesema, kwa sasa Viwanda vinaitaji ngozi zenye kukidhi Viwango hivyo kutambulika kwa wachunaji wa ngozi kutasaidia kwa kiasi kikubwa Uzalishaji kuongezeka.

“Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 45 hadi 65 ya wachunaji wa ngozi wamekuwa wakichagia uharibifu wa ngozi hivyo tumeona kundi hili ni muhimu kulipa mafunzo kama haya,”amesema Bura.

Salumu Abdallah ni mmoja wa wachunaji wa ngozi waliopata leseni amesema mafunzo aliyoyapata yatamsaidia kwa kiasi kikubwa kufanya kazi yake kwa viwango vya ubora tofauti na awali.