March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuboresha Ushauri kwa Taasisi za Umma wakati wa kuingia mikataba

Na Penina Malundo,Timesmajira

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuboresha Ushauri kwa Taasisi za Umma wakati wa kuingia mikataba mbalimbali ili kuwa na Mikataba iliyobora na kutimiza malengo ya Serikali ya kuwa na mikataba inayotekelezwa vizuri na kuwanufaisha Wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Samwel Maneno katika Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Amesema wanaendelea kuzipa ushauri Taasisi za Umma ili kuwa na ubora wa mikataba pia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Mikataba hiyo unafanyika kwa mujibu wa Makubaliano.

Amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayatumia maonesho hayo katika kutoa Ushauri wa Kisheria, Kushughulikia Malalamiko, Utatuzi wa Migogoro na Elimu ya Sheria hususani sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 zilizoanza kutumika Julai 1, 2025.

“Sheria zilizofanyiwa urekebu zimezinduliwa na zimeanza kutumika na kitu kizuri ni kuwa kati ya sheria 446 sheria 300 zinapatikana kwa lugha ya kiswahili”,amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Amesema Serikali imesema kuwa moja ya mambo makubwa ambayo ofisi hiyo inafanya ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia mikataba ikiwemo ya uwekezaji na ujenzi.

“Mikataba yote wanayosimamia na ofisi hiyo inahusisha fedha nyingi kwa Serikali ambazo zinapatikana kwa mujibu wa bajeti na kodi za wananchi ili adhima ya serikali iweze kutimia lazima kuwe na mikataba mingine ambayo utekelezaji wake hautakuwa na changamoto yoyote ili kusudio lililokusudiwa na serikali liweze kutimia.

“Hivyo kuna ubora wa mikakati wa mikataba na hivyo sasa inafanyika kwa mujibu wa makubaliano na tunahakikisha migogoro yoyote inayojitokeza katika mikataba inapata suluhu ya mapema ili kuepusha kuwa na migogoro endelevu kukwamisha utekelezaji wa mikataba hiyo mwisho wa siku serikali kushindwa kutimiza malengo yao na wananchi kukosa huduma ambazo serikali imepenya iwafikie wananchi kwa wakati,”amesema .

Katika hatua nyingine Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitembelea mabanda ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria pamoja na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, kuona shughuli zinazotekelezwa na Taasisi hizo katika maonesho hayo.Maonesho ya Sabasaba 2025 yamezinduliwa rasmi leo tarehe 7 Julai, 2025 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo maonesho yanatarajiwa kumalizika tarehe 13 Julai, 2025.