January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Mkoa,TRA yaungana kushughulikia wasiolipa kodi

Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online Bukoba,

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amesema kuwa uongozi wa Mkoa umeungana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine za wafanyabiashara mkoani humo kutafuta njia bora na kuunda kikosi maalumu ambacho kitakabiliana na wafanyabiashara ambao wamekuwa kero katika suala la kutolipa kodi.

Mwassa ametumia saa zaidi ya sita katika usiku wa pamoja na wafanyabiashara kutoka Halmashauri nane za mkoa wa Kagera na kuelezea umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.

Pia ametumia fursa hiyo kueleza madhara ya kukwepa kulipa kodi huku akitoa pongezi kwa wafanyabiashara wote walioibuka na tuzo,zawadi na vyeti kwa ulipaji bora wa kodi kwa kipindi cha mwaka mzima.

Amesema kuwa kikosi hicho kitatafuta njia bora na salama ya kuwakabili wafanyabiashara ambao wamekuwa kikwazo kwa kutolipa kodi ambacho kitakuwa na mchanganyiko wa watumishi wa TRA na serikali ,Jeshi la Polisi olisi, taasisi za biashara.

” Nachukua nafasi hii kuwaponageza wafanyabiashara mkoani Kagera ambao mmekuwa mkilipa kodi kwa hiari,bila shaka mnaona faida nyingi za kulipa kodi, maendeleo ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita,tulipe kodi ndugu zangu ,kulalamikia uchache wa maendeleo bila wewe kujitikisa na kuchangia chochote huo ni uwenda wazimu,”amesema Mwassa

Akitoa taarifa za makusanyo ya kodi kwa miaka tofauti tofauti Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera Mwita Ayoubu amesema kuwa Mkoa huo umeendelea kufanikiwa kupiga hatua na kuvuka asilimia ya kiwango kinachokusanywa na ndani ya robo ya mwaka wa fedha 2023/2024 asilimia 98 ya makusanyo imefanikiwa.

Amesema kuwa uhusiano wa wafanyabiashara na wafanyakazi wa TRA umeimarika na ulipaji wa kodi kwa hiari umeongezeka na hakuna fungafunga ya maduka ya wafanyabiashara huku elimu ya kulipa kodi ikieendelea kutolewa kila mara.

Kwa niaba ya Kamishina Mkuu wa TRA makao makuu Ramadhan Sengati amesema kuwa tatizo la kutumia mianya ya vichochoro kukwepa kodi Mkoa wa Kagera bado ni kubwa,shughuli za magendo na wafanyabiashara wanaotumia Ziwa Victoria kutorosha bidhaa au kuingiza bidhaa kinyume na sheria bado ni kubwa pia hivyo serikali inapaswa kuongeza nguvu katika kikosi kinachoundwa na Mkuu wa Mkoa.

Hata hivyo amesema kuwa ujio wa meli ya mizigo itakayofanya safari zake katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria itaongeza wigo wa makusanyo.