January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Bunge kuja na Bunge Bonanza

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

OFISI ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza ujio wa Bunge Bonanza ambalo litahusisha Michezo mbalimbali litakalofanyika Jijini Dodoma Januari 28, 2023 likiwa na lengo la kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Kisukari, Shinikizo la damu na Uzito uliopitiliza.

Huku  Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Ujio wa bonanza hilo umetangazwa,jijini hapa leo,Januari 26,2023 na Spika wa Bunge hilo Dkt.Tulia Ackson ambapo ametaja lengo lingine kuwa

ni kutoa fursa ya kukutanisha waheshimiwa wabunge, watumishi na wadau mbalimbali katika Mazingira rafiki ya nje na Ofisi ili kufahamiana na kujenga Umoja utakaosaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Natarajia watumishi wa bunge na waheshimiwa wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi watajiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuimarisha mifupa na misuli, kuongeza uhimili, utimamu wa mwili na hatimaye kuwa na afya njema,”mesema Dkt. Tulia.

Amesema bonanza hilo litaanza kwa matembezi yatakayoanzia Chuo cha Mipmngo na kuishia shule ya sekondari ya John Merlin ambapo ndipo litakapofanyikia na miongoni mwa michezo itakayo husishwa siku hiyo ni pamoja na Mpira wa miguu, kukimbia na maji,Mpira wa kikapu, Mpira wa wavu, Kurusha vishale na riadha.

“Kutakuwepo na mchezo wa mpira wa meza, kutembea kwa haraka, bao, draft, kuvuta kamba kufukuza kuku, kukimbia kwa kijiko, kukimbia na glass ikiwa na maji, kushindana kunywa soda na kula chakula kwa haraka,”amesema Dkt. Tulia.

Wabunge, Watumishi wa Bunge na Wadau mbalimbali kutoka Tanzania bara na Visiwani Zanzibar watashiriki bonanza hilo linalokwenda na kauli mbiu ya, “Bunge Bonanza; “Shiriki Michezo, Jenga Taifa lenye Afya”