December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyumba ya watumishi kuboresha
utoaji huduma Zahanati Wikichi

Na Mwandishi wetu, Njombe

NYUMBA ya watumishi (two in one) inayojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mtaa wa Wikichi, Kata ya Ramadhani Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, itakapokamilika itawezesha wananchi wa mtaa huo kupata huduma za afya kwa saa 24 tofauti na hali ilivyo kwa sasa ambapo zinakomea saa 9.30.

Zahanati hiyo ya Wikichi imejengwa na TASAF kwa gharama za sh. milioni 89 na wananchi wa mtaa huo kuchangia nguvu kazi kwenye ujenzi huo kwa asilimia zisizopungua 10.

Zahanati hiyo ilianza kutoka huduma 2021, lakini kukaibuka changamoto ya kushindwa kutoa huduma kwa wananchi kwa saa 24 kutokana na kukosena kwa nyumba ya watumishi.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika kwenye zahanati hiyo na kujionea maendeleo ya miradi hiyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Wikichi, Oden Lwihisa (48) amesema ujenzi wa nyumba hiyo ya watumishi huko juu ya lenta.

Lwihisa amesema baada ya kujitokeza fursa ya miradi ya TASAF kwenye mtaa wao, wananchi kupitia mkutano wa mtaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2019, waliibua mradi wa ujenzi wa zahanati.

Amesema ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwaka 2020 na Julai, 2021 ulikamilika na Septemba, 2021 ndipo huduma zilianza kutolewa. Amesema pamoja na idadi ya wananchi katika mtaa cha Wikichi kuwa ndogo, lakini walionesha mwitikio mzuri uliowezesha ujenzi wa zahanati hiyo kukamilika kwa wakati.

Amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa zanahati hiyo na kuanza huduma, ndipo Agosti, mwaka jana walitakiwa wachague mradi wa kipaumbele kati ya wodi ya wazazi na nyumba ya wafanyakazi wa zahanati hiyo.

Lwihisa amesema wananchi walipokutana kwenye mkutano waliona kipaumbele kiwe nyumba ya wauguzi ili wagonjwa wawe wanapata huduma kwa saa 24.

Ujenzi wa nyumba ya watumishi (two in one) ukiendelea katika Zahanati ya Wikiti iliyopo Kata wa Ramadhani Halmashauri ya Mjini Njombe

Hivyo mwaka jana TASAF iliwakubalia kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi (two in one) ambapo wananchi wanachangia mradi huo kwa asilimia 10.

Amesema wanachangia asilimia 10 kwa kuandaa mawe na tofari huku fedha za mradi zikianza kufanyakazi kuanzia ujenzi wa msingi, ukuta, kupaua hadi finishing . “Mbali na kuandaa mawe na tofari, huwa tunakuja kuwasaidia mafundi shughuli zinazokuwa zinaendelea ikiwemo kuwasogezea mawe, mchanga na wao ndio walioshiriki kuchimba msingi,” amesema Lwihisa.

Amesema mbali ya wananchi kujitolea kwenye ujenzi wa nyumba hiyo kuna wadau wengine walijitokeza kusaidia ujenzi huo ambao ni Kanisa Katoliki waliowasaidia mawe lori tano, mbunge pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema anampongeza Rais Samia Sulumu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, kwani miradi mingi wanaiyona nchi nzima kwenye vyombo vya habari. “Ndiyo maana hata kwenye mtaa wangu wananchi wanajua wanapewa miradi kwa ajili ya huduma za jamii,” amesema.

Naye mtunza stoo katika mradi huo, Chesco Mlondelwa, alisema TASAF iliwapatia sh. milioni 66 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi. Amesema kama mtunza stoo hakuna vifaa vya ujenzi vinavyotolewa kwa ajili ya ujenzi mradi pasipo na umuhimu, na anahakikisha vinapotoka vinaenda kwenye kazi iliyokusudiwa.

Amesema akishatoa vifaa stoo kwenye eneo la mradi kunakuwa na mjumbe wa kamati ya ujenzi anakuwa eneo la mradi ili kusimamia vifaa vilivyotoka stoo vimetumika inavyotakiwa na kama vikibaki vinarudishwa stoo.

Anasema maendeleo ya mradi ni mazuri ambapo kwa sasa upo kwenye hatua za kufunga lenta.

Zahanati ya Wikichi

Naye fundi mkuu katika mradi wa jengo hilo, Vasco Hyera amesema mradi huo unaendelea vizuri na kwa sababu ana vijana wa kutosha ana imani utafanyika kikamilifu.

Amesema miradi ya aina hiyo ina faida kwa wananchi na hata kama zikitokeza changamoto anakuwa anajua kwamba hiyo ni sehemu ya kawaida kwenye miradi yote, kikubwa anachotaka kuhakikisha ni ubora unaotakiwa.