Na Thomas Kiani, Timesmajira Online, Singida
MWANAMKE mmoja mkazi wa Kijiji cha Mtunduru Kata ya Mtunduru Tarafa ya Sepuka Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, Asha Saidi Mngeja (77) amefariki katika kituo cha Afya Sepuka alipofikishwa ili kupatiwa matibabu kwa kile kinachoelezwa kuumwa na nyuki wakati akitoka mashineni kusaga.
Akitoa taarifa juu ya tukio hilo, ndugu wa karimu wa marehemu hiyo, Abdi Isumail Mtonka amesema, tukio hilo lilitokea jana saa 11:00 ambapo wakati Asha anatoka kusaga alikuta mzinga wa nyuki umeanguka huku nyuki wote wakiwa wamesambaa aneo hilo.
“Mzinga ulipoanguka ulipasuka na masega yote yakamwagika chini na nyuki waliokuwemo kwenye mzinga huo waliruka wakasambaa eneo lote na kwa bahati mbaya wakamkuta bibi huyo na kuanza kushambulia, alianguka chini na kupiga mayowe na kitendo hicho kilipelekea nyuki kuingia hadi mdomoni,” amesema Mtonka.
Amesema, kwa bahati nzuri kelele alizopiga zilifanya watu kufika ili kutoa msaada lakini walikuta mwili wote umejaa nyuki waliokuwa wanamuuma na mwili wake wote ulijaa miiba ya nyuki hivyo walimkimbiza zahanati ya Kijiji Mtunduru ili kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Sombi Mangu amesema, baada ya Asha kufikishwa Zahanati, Daktari alisema, sumu ya nyuki imeenea mwili na kushauri akimbizwe haraka kituo cha Afya Sepuka kwa matibabu zaidi lakini ilipofika saa 3:00 Usiku akafariki.
Taarifa iliyotolewa na Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Yessaya Mwandigo imesema kuwa, bibi huyo amepoteza maisha baada ya kufikishwa hospitalini hapo kutibiwa na kwa mujibu wa uchunguzi wa awali umeonesha kifo chake kimetokana na sumu ya nyuki kuzidi mwilini.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja