Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RASMI klabu ya Yanga imetangaza kuachana na nyota wake 14 kuelekea kwenye maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).
Wachezaji ambao wameachwa huru baada ya mikataba kuisha ni pamoja na Mrisho Ngassa, David Molinga, Jafary Mohammed, Tariq Seif, Andrew Vicent, Nahodha Papy Kabamba Tshishimbi na Mohammed Issa ‘Banka.’
Wachezaji ambao klabu inazungumza nao ili kusitisha mikataba yao ni Ali Mtoni, Muharami lssa Maundu, All Ali, Yikpe Gislain, Patrick Sibomana, Eric Kabamba na Rafael Daud.
Wachezaji hao wameachwa baada ya kikao kilichofanyika jana baina ya viongozi na wachezaji huku sababu kubwa za wachezaji hao kuachwa ikitajwa kuwa ni nidhamu mbovu na kuonesha viwango duni.
Kabla ya kuweka wazi orodha hiyo ya wachezaji 14, awali ilitoka orodha ya wachezaji 19 ambao wangeacha kutokana na sababu hizo kubwa mbili za nidamu na viwango visivyoridhisha.
Lakini licha ya kuachana na nyota hao, Yanga imewabakiza Farouk Shikhalo ambaye awali alichajwa kuachwa kutokana na kiwango chao kutowaridhisha viongozi, Ramadhan Kabwili, Metacha Mnata, Haruna Niyonzima, Lamine Moro na Bernard Morrison.
Wengine ni Feisal Salum, Juma Mahadhi, Adeyum Saleh, Said Juma Makapu, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi, Abdullaziz Makame na Paul Godfrey huku pia klabu ikiendelea na mazungumzo na wachezaji wake wakongwe, Juma Abdul na Kelvin Yondani ambao mikataba yao imeisha ili kuendelea kuitumikia timu ya Wananchi.
Wengi wa wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga wamepongeza maamuzi hayo lakini wameshangazwa na uongozi wao kumbakiza Morrison ambaye hivi karibuni alikuwa na mgogoro na viongozi juu ya suala la mkataba hali iliyosababisha kesi kuepelekwa ndani ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Mbali na sintofahamu hiyo lakini pia Morrison alionesha nidhamu mbovu jambo lililofanya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kushikiza uongozi kuachana naye kwa kile walichokitafsiri kuwa anawapanda viongozi kichwani.
Akitolea ufafanuzi wa jambo hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema Morrison ataendelea kusalia ndani ya klabu hiyo kwani bado wanamkataba naye.
Wakati Yanga ikiachana na wachezaji hao tayari wameshafanya usajili wa wachezaji kadhaa ili kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi ambao wanahitaji kutwaa mataji.
Mbali na usajili huo ambao umeshafanyika, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ameliambia Majira kuwa, usajili utakaoendelea baada ya kuchukua maamuzi hayo utawashangaza wengi kwani watashusha wachezaji wenye uwezo mkubwa na wenye hadi ya kuitumikia Yanga ambao wanaamini watawafikisha kwenye malengo yao.
“Unajua toka tulipopoteza matumaini ya kutwaa kombe la Ligi na lile la Shirikisho, mipango yetu ilikuwa kufanya usajili mkubwa na si wa kuongeza nguvu kama wengi walivyotamani ili kufika tunapopataka kwa kuleta wachezaji ambao watapambana kutufikisha tunapopahitaji,” amesema kiongozi huyo.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025