December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyanhembe FC kukiwasha dhidi ya Ndugu FC,kuipongeza Taifa Stars

Na Suleiman Abeid,
Timesmajira Online, Shinyanga

TIMU za Nyanhembe FC na Ngudu FC za kata ya Kilago wilayani Kahama mkoani Shinyanga zinatarajiwa kumenyana vikali katika mchezo maalumu wa kirafiki kwa ajili ya kuipongeza timu ya Taifa Stars kwa kufanikiwa kucheza fainali za mataifa ya Africa (AFCON) mwaka 2024.

Kwa mujibu wa mwandaaji wa mechi hiyo ya kirafiki ambayo imeonesha kuwavutia wapenzi wengi wa michezo wa kata ya Kilago na kata jirani, mchezo huo utafanyika Jumatano ya Septemba 13, mwaka huu katika uwanja wa mpira wa Kilago Manispaa ya Kahama.

Mwandaaji huyo Mnyama Nzumbi amesema mgeni rasmi katika mchezo huo atakuwa ni mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoani Shinyanga (SHIREFA) Khamis Mgeja ambaye pia ni mmoja wa wadau wakubwa wa mchezo wa mpira wa miguu mkoani Shinyanga.

Nzumbi amesema yeye binafsi amefurahishwa sana na kitendo cha timu ya Taifa Stars kufanikiwa kutinga kwenye michuano ya fainali za kombe la Mataifa huru ya Afrika (AFCON) michuano ambayo itachezwa huko nchini Ivory Coast mwezi Januari 2024.

“Nimefurahishwa na kitendo cha timu yetu ya Taifa kutinga fainali za AFCON, sasa kwa furahi hii nimeona niandae mchezo maalumu wa kirafiki kati ya timu zetu za kata ya Kilago ili ziweze kucheza mchezo wa kuipongeza timu yetu,”

“Naamini matokeo hayo ya Taifa Stars yamewafurahisha watanzania wengi, hivyo ni vizuri na wengine wakaiga mfano kwa kuandaa michezo mbalimbali ya kuipongeza timu yetu, hii itachangia kuwapa moyo na kuwajengea imani wachezaji kwamba sisi watanzania wenzao tunawaunga mkono,” ameeleza Nzumbi.

Kwa upande wake Khamis Mgeja ambaye amealikwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo amesema ameupokea kwa mikono miwili mwaliko huo na kwamba kitendo kilichofanywa na mdau huyo wa michezo ni cha kizalendo na kinastahili kupongezwa.

“Huu ni uamuzi wa busara na wa kizalendo, naamini utatoa hamasa kubwa kwa vijana wetu wa Taifa Stars mwakani kwenye michezo ya fainali hizo za AFCON, na ili waweze kufanya vizuri ni vyema watanzania wote tukaungana kwa sasa mbali ya kuwapongeza pia tuwape moyo ili wakafanye vizuri,”

“Binafsi nilifarijika sana siku ambayo timu hiyo iliweza kusimama kidete kule Algeria na kutoka sare tasa na timu ya Taifa hilo na hivyo kufanikiwa kuingia fainali mwakani, ukweli wamepambana na wanastahili kupongezwa na kila mtanzania, nashauri watu waige pia mfano huyo mdau wa michezo, Mnyama Nzumbi alivyofanya,” ameeleza Mgeja.

Mgeja licha ya mdau mkubwa wa michezo nchini pia amekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha michezo nchini hasa kwenye masuala mazima yanayogusa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla ikiwemo kusaidia timu za mpira wa miguu na kwa sasa anasimamia kituo cha Kahama United Sports Academy (KUSA).