January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyamagana yazindua kampeni ya chanjo ya surua, rubella

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Halmashauri ya Jiji la Mwanza limezindua kampeni ya chanjo ya surua rubella kwa watoto wenye umri wa miezi tisa hadi miaka minne na miezi kumi na moja(miezi 59),huku wazazi wakihimizwa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo kwani ni salama.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao kiwilaya,Wilaya ya Nyamagana umefanyika kituo cha afya Makongoro,kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala ameeleza kuwa afya ni wa binadamu,hivyo wazazi wahakikishe watoto wao wanapata chanjo hiyo kwa ajili ya ustawi wa taifa la kesho.

Ameeleza kuwa serikali imejipanga kwa kuleta dozi za kutosha kwani katika kampeni hiyo wanatarajia kuwafikia watoto zaidi ya 80,000, hivyo wazazi waendelee kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na waachane na maneno ya upotishaji huko mitaani.

“Tufuate maelekezo tuwapatie watoto chanjo ambao kimsingi wanatutegemea sisi wazazi na walezi,hivyo niwasihi sana waambieni wazazi wengine na walezi pia kuwa chanjo hii ni salama,bure na masharti yake kimsingi ni umri wa mtoto,”ameeleza Salala.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sebastian Pima, ameeleza kuwa kampeni hiyo ni ya siku nne inayoanza leo Februari 15 hadi 18 mwaka huu.

Dkt.Pima ameeeleza kuwa wamelenga kuwafikia watoto zaidi ya 80,000 na chanjo hiyo ni salama na itatolewa kwa watoto wenye umri wa miezi tisa hadi miaka minne na miezi kumi na moja.

Naye mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake amepata chanjo hiyo Irene Shukrani, ameeleza kuwa chanjo ni salama na anaamini ni kinga kwa watoto kutokupata magonjwa hayo kwani tangu anakuja hajawai kusikia mtu au mtoto aliyepata madhara kutokana na chanjo hizo.