November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyabundege aanza kazi rasmi TADB kwa kuahidi matokeo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar

MKURUGENZI Mtendaji mpya wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege ameanza kazi na kuahidi matokeo na kuwataka wafanyakazi wa benki hiyo kumpa ushirikiano na kufanya kazi kiuweledi sambamba na kuleta mageuzi makubwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.

“Napenda kuona kila mfanyakazi anafanya kazi kwa ari mpya,kasi mpya na nguvu mpya ili kufanikisha malengo ya benki ya kuleta mageuzi kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Nyabundege.

Akizungumza na wafanyakazi waliomkaribisha jijini Dar es Salaam jana kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo, hivi karibuni, Nyabundege ambaye amebobea katika masuala ya benki na kifedha , amesema TADB ni chombo muhimu katika kuleta mapinduzi kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na hivyo amejipanga kuhakikisha benki hiyo itafikia malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu uundwaji wake.

“Nitahakikisha malengo yote yanatekelezwa kikamilifu sambamba na kuziwezesha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ziweze kutoa mchango stahiki katika kujenga uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa,” amesema huku akishangiliwa na wafanyakazi waliokuwa wamejawa furaha.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo muda mfupi baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza juzi Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo hiyo hivi karibu.

Ameeleza kuwa TADB ina nafasi kubwa ya kupelekea mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuhakikisha wakulima wadogo wanapatiwa mikopo na elimu juu ya kuongeza tija katika uzalishaji na thamani ya mazao.

Nyabundege amesema ni ukweli usiopingika kwamba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wamejiajiri au kujihusisha moja kwa moja shughuli za kilimo, hivyo TADB ni lazima iwainue zaidi kwa kuwapa mikopo.

“Tija katika uzalishaji mazao itakapoongezeka itachochea uanzishwaji wa viwanda vingi vya kuchakata mazao nakupelekea ongezeko la ajira kwa vijana hali itakayosaidia kupunguza tatizo la upatiakanaji wa ajira nchini,” amesema Nyabundege.

Amesema usalama wa chakula nchini unategemea katika uzalishaji wenye tija, hivyo TADB itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha uzalishaji wa mazao unaongezeka na kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza nje ya nchi.

Katika hatua nyingine alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuingoza benki hiyo ambayo ina dhamana ya kutoa mikopo kwa wakulima na kuhakikisha mnyororo wa thamani wa mazao katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi unaboreshwa.

“Ni heshima kubwa kuteuliwa na kiongozi mkuu wa nchi hii ni hamasa kwangu katika kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kujitoa zaidi ili kufikia malengo ya Serikali kwa kulifanya taifa letu kuwa katika uchumi wa viwanda,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege (kulia) akikaribishwa na wafanyakazi wa benki alipowasili kwa mara ya kwanza juzi Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo hiyo hivi karibu.

Aidha, Nyabundege amewataka watendaji wote katika benki hiyo muhimu kumpa ushirikiano ili kufikia malengo na faida ya kuwepo kwa benki hiyo ikawanufaishe wengi kwa kuhakikisha mageuzi makubwa yanafanyika katika sekta za kilimo,mifugo na uvuvi.

Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, Nyabundege alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Lake Oil Tanzania Limited na vile vile ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika sekta za kibenki. Aliwahi pia kuhudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa TIB Corporate Bank Tanzania Limited.

Mpaka sasa benki hiyo imeshatoa mikopo ya zaidi ya sh. bilioni 300 katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini.