Na Penina Malundo, Timesmajira
MKUU wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii kutoka Manispaa ya Kinondoni,Alex Ntiboneka ametoa wito kwa mashirika yanayofanya shughuli za uwezeshaji wa vijana na wanawake kuwekeza katika kubadilisha fikra za vijana juu ya kufanya kazi na kuhamasisha vijana kutoka vijiweni na kuachana na shughuli ambazo sio rasmi.
Akitoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa warsha ya siku moja kwa vijana wa vyama mbalimbali iliyoandaliwa na Shirika la Mazingira,Haki za Binadamu na Jinsia( Environcare),amesema vijana na wanawake wanatakiwa wajiiingize katika masuala ya uzalishaji na kwenda katika manispaa zao kuchukua mikopo na kujikita katika kuzalisha na kurudisha mikopo.
Amesema serikali inatoa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu kwasababu inalenga kuwaandaa kundi hilo katika nafasi ya uongozi .
Amesema masuala ya uongozi yamekuwa na vikwazo kwa vijana na wanawake ambavyo vimepelekea kushindwa kushiriki au kushirikishwa katika masuala ya uongozi.”Vikwazo vingi tayari vimefanyiwa kazi ila katika suala la uwezo wa kiuchumi kwa vijana,wanawake bado.

”Tunatakiwa kupunguza wimbi la vijana wengi kukaa bila shughuli za kufanya na ili kijana au Wanawake kugombea nafasi hizi hatua ya kwanza kugombea au kushiri nafasi ya uongozi ni lazima awe na shughuli ya kufanya,”alisema.
Amesema kijana au wanawake wanapokuwa vizuri kiuchumi hata hali ya kujiamini ya kwenda kuchukua fomu au kuamua kugombea inakuwa kubwa ukilinganisha na mtu ambaye hana shughuli ya kufanya,mzurulaji au tegemezi anakuwa mzigo kwa taifa .
”Kila kijana akiitikia wito huu na kutumia fursa hizi zilizoandaliwa na Serikali akiwezeshwa kiuchumi anaweza kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi zinazokuja ambapo mwaka jana kulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka huu uchaguzi mkuu ambapo tutachagua madiwani,Wabunge na Rais kwahy ni nafasi kwa vijana kujitokeza kushiriki lakini ukiwa na uchumi imara,”amesema.
Aidha kundi la Vijana na Wanawake nchini linatakiwa kuitikia wito wa kutumia fursa za kiuchumi zilizowekwa na serikali ili kuwaimarisha na kuwaandaa kwenye nafasi ya uongozi.

Kwa upande wake Meneja wa Miradi wa Envirocare,Godlisten Muro amesema kwa sasa wanaendesha mradi maalum wa ushiriki wa wanawake pamoja na vijana katika masuala ya uongozi.”Mradi huu wa miezi 21 unafadhiliwa na shirika la Forum CIV lenye makao makuu nchini Sweden,wenye lengo la kutoa elimu kwa wanawake na vijana kuhamasisha kushiriki katika masuala ya uongozi.
”Hadi sasa tumefikia takribani vijana 300 ambapo wamepewa mafunzo ya uongozi na washiriki hao wameonekana kujiamini na kushiriki vizuri katika masuala ya uongozi,”amesema.
Amesema pamoja na mada mbalimbali wataangalia namna ya kuwawezesha kiuchumi kutumia fursa mbalimbali za kiserikali zilizopo ikiwemo mikopo ya halmashauri itawawezesha kiuchumi na kuwa viongozi wazuri.
”Kwa kweli suala la uongozi linaendana sambamba na suala la kiuchumi sababu ni lazima kuna gharama za uchaguzi,kugombea hivyo vijana kama hawapo vizuri kiuchumi wataadhiri sana suala ya uongozi.
”Hii ni Changamoto kubwa ambayo tumeiona kwani wazee wengi wanaendelea kuwa viongozi kutokana na fedha walizonazo ambapo inawaathiri sana vijana na vijana wakiwa na nguvu ya kiuchumi wanaamini kwamba itasaidia kushiriki katika uongozi,”amesisitiza.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Emanuela Andrea amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana kwasababu wanajifunza kwani suala la vijana na wanawake katika suala la uongozi linachangamoto nyingi.
”Kikubwa vijana tunatakiwa kupambana na kujiamini ili kupata nafasi muhimu za uongozi licha ya changamoto mbalimbali kujitokeza ikiwemo masuala ya kiuchumi,”amesema
More Stories
Child support Tanzania yapongezwa kutetea maslahi watoto wenye ulemavu
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.Â
Samamba:Uongezaji thamani madini ni mkakati wa serikali kukuza mchango wa sekta