Na Mwandishi Wetu, TimesMajirra,Online
WAKATI wa kuelekea kilele cha siku ya Wanawake Duniani Machi 8, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeguswa na kutoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Msaada wa vifaa tiba hivyo ambavyo ni vitanda vya kujifungulia akina mama pamoja na mashine za kupimia shinikizo la damu vilikabidhiwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele kwa Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Msafiri Marijani.
Lulu amesema Mfuko umetoa msaada huo ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8, mwaka huu ikiwa na kauli mbiu isemayo ‘Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu’.
Akipokea msaada huo Dkt. Marijani amesema kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Zanzibar, wanaishukuru NSSF kwa kutoa vifaa tiba hivyo ambavyo vitatumika katika kuokoa maisha ya wananchi wanaokuja kupata huduma.
Dkt. Marijani amesema wamepokea msaada huo kipindi ambacho mahitaji ya vifaa tiba katika hospitali hiyo ni makubwa mno licha ya Serikali kujitahidi kununua vifaa vya kutolea huduma lakini mapungufu yaliyopo wanaendelea kuungwa mkono na wadau kama NSSF.
“Tunawashukuru NSSF kwa kutupatia msaada huu ambao unaenda kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopata huduma katika hospitali yetu nina wahakikishia kuwa vifaa hivi vitatumika kwa lengo lililokusudiwa,” amesema.
Hata hivyo, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele amesema baada ya kupata uhitaji wa vifaa tiba kutoka kwa uongozi wa hospitali hiyo, Mfuko uliamua kuwaunga mkono kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia katika kuokoa maisha ya wagonjwa.
“NSSF kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu tunaendelea kuwashukuru wenzetu wa ZSSF (Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar) kwa mashirikiano ya Mifuko hii pamoja na Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kukubali kupokea vifaa tiba hivi ambavyo vitatumika kuwahudumia wagonjwa mbalimbali,” amesema.
Lulu amesema Mfuko pamoja na kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao pia unachangia shughuli mbalimbali kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla kwa kuwajibika katika jamii (CSR) hasa katika maeneo ya afya, elimu, michezo, jamii na kudhamini shughuli mbalimbali za wadau.
Mwenyekiti wa Wanawake NSSF, Vaileth Segeja, amesema wametoa msaada huo kwa sababu Mfuko una sera ya kutoa msaada katika jamii, na kutoa wito kwa wanawake wote waliopo katika sekta isiyo rasmi kujiunga na Mifuko ya hifadhi ya jamii ukiwemo wa NSSF na ZSSF kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye.
Kwa upande wake, Nassor Hassan ambaye ni Afisa Utawala wa ZSSF amesema kazi kubwa ya Mifuko ya hifadhi ya jamii ni kuihifadhi jamii pale inapopata janga ikiwemo ugonjwa na ndio maana NSSF iliamua kutoa msaada wa vifaa tiba hivyo ili vikasaidie kuokoa maisha ya wananchi.
Alisema NSSF na ZSSF wana mashirikiano ya muda mrefu katika kusaidia baadhi ya shughuli kama kuhakiki wanachama na kwamba wataendelea kushirikiana kwa mustakabali wa Taifa na jamii kwa ujumla.
MWISHO
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi