January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wakifuatilia huduma za NSSF

NSSF yakusanya mil.447/- kupitia One Stop Jawabu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dar

ZAIDI ya sh. milioni 447 zimekusanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kipindi cha wiki mbili kutoka kwa waajiri ambao walikuwa hawajawasilisha michango ya wafanyakazi wao kupitia maonesho ya kutatua kero za wananchi wa Wilaya ya Temeke ‘ ‘One Stop Jawabu”.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Rebule Maira, alisema maonesho hayo yaliandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi hasa wa kawaida ili kuhakikisha wanapata uelewa mpana kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za Serikali.

Maira alisema kupitia maonesho hayo Shirika limewahudumia wananchi zaidi 480 kati ya hao 60 wamejiunga na NSSF kupitia Sekta isiyo rasmi inayohusu wafugaji, wakulima, wavuvi, wachimbaji wadogo, mamalishe na bodaboda.

Alisema kupitia maonesho hayo, NSSF ilikuwa inatoa elimu kwa wananchi namna mafao yanavyotolewa na kwamba huduma zilizo kuwa zinatolewa katika maonesho hayo ni zile ambazo zinatolewa kwenye ofisi zote za Shirika zilizopo maeneo yote nchini.

“Kupitia One Stop Jawabu, Shirika letu limepata mafanikio makubwa ikiwemo kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wa kawaida ambao wamejiunga na kuanza kujiwekea akiba yao ya baadaye,” alisema.

Alisema NSSF inatekeleza kwa vitendo maelekezo yote ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kuwahudumia wananchi wa kawaida kupata huduma bora karibu na maeneo yao ikiwemo huduma za Hifadhi ya jamii.

Maira aliwaomba waajiri wote nchini, ambao hawajapeleka michango ya wafanyakazi wao kuipeleka kwa wakati kwani kutopeleka michango ni kosa kisheria.