.Ni kwa wenye malimbikizo ya michango, muitikio wazidi kuwa mkubwa
Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), unaendelea na kampeni yake ya msamaha wa tozo ambayo inalenga kuwahamasisha waajiri wote wa sekta binafsi kulipa michango yao ili kuondokana na tozo zinazowakabili.
Katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) kwenye kipengele cha kampeni ya mwezi, Mshomba amesema kampeni hiyo ya kuwahamasisha waajiri kulipa michango yao ilianza mwezi Oktoba, 2021 na inahusu waajiri wote wa sekta binafsi wenye malimbikizo ya michango kwa kipindi kilichoishia Juni 30, 2021.
“Katika kipindi hicho waajiri wote waliolipa malimbikizo ya michango yao kuanzia Oktoba 1, 2021 mpaka Novemba 30, 2021 walinufaika na msamaha wa tozo kwa kiwango cha asilimia 100,” amesema Mshomba.
Pia, waajiri wote waliolipa malimbikizo ya michango kuanzia Desemba 1, 2021 mpaka Desemba 31, 2021 walipatiwa msamaha wa tozo kwa kiwango cha asilimia sabini na tano.
Kwa mujibu wa Mshomba, waajiri wote watakaolipa malimbikizo ya michango yao kuanzia Januari 1, 2022 hadi Januari 31, 2022 watapata msamaha wa tozo kwa kiwango cha asilimia 50.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF, ameweka wazi kuwa lengo la Mfuko kuja na msamaha huo ni kuwaondelea mzigo waajiri kwani tozo hizo ni kubwa na ni mzigo kwa mwajiri huku akisisitiza kuwa, msamaha huo pia unalenga kuboresha mazingira ya biashara zao kwa kuwa fedha ambayo walipaswa kulipa kama tozo wataitumia katika shughuli zingine za maendeleo ya taasisi zao.
“Msamaha huu unawafanya waajiri kutumia fedha hizo ambazo wangelipa tozo katika shughuli nyingine za kiuchumi na uzalishaji na kuongeza kipato cha kampuni zao,” amesema Mshomba.
Mshomba amefafanua kuwa, tozo zinasababishwa na waajiri wenyewe kwa kutolipa michango kwa wakati kama sheria inavyosema, ambapo alitoa wito kwa waajiri kuchangamkia fursa hiyo ndani ya mwezi huu wa Januari ili waweze kupata msamaha kwa asiliamia 50.
Ameainisha kuwa, NSSF imeweka kipaumbele katika kuelimisha waajiri wa sekta binafsi na umma kwa ujumla kuhusiana na msamaha huo pamoja na umuhimu wake ili waweze kuelewa vizuri.
Mshomba alitumia fursa hiyo kuwasisitiza waajiri kwenye sekta binafsi nchi mzima kuwasilisha michango yao kwa mujibu wa sheria na kuepuka kukumbana na tozo.
Katika hatua nyingine, Mshomba aliweka wazi kuwa tokea kuanza kwa kampeni hiyo ya msamaha wa tozo muitikio umekuwa mkubwa ambapo NSSF imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 17, fedha ambazo isingepatikana bila ya msamaha huo.
Mshomba ameendelea kubainisha kuwa fedha za wanachama wa NSSF zipo salama na Mfuko unazidi kukua ambapo hivi sasa thamani ya Mfuko imefikia sh. trilioni 5.4 na makusanyo ya mwezi yameongeza kufikia wastani wa sh. bilioni 113 kwa Desemba, mwaka jana 2021, kiasi ambacho hakijawahi kutokea.
More Stories
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume