June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NSSF kupunguza changamoto ya uhaba wa Sukari nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii(NSSF )imesema kuwa kufikia Julai mosi mwaka huu tayari itakuwa imeweza kuzalisha sukari kupitia kiwanda cha sukari cha Mkulazi.

Kiwanda hicho kimeelezwa kuwa kitapunguza changamoto ya uhaba wa sukari inayojitokeza mara kwa mara na kulazimu serikali kutegemea wazalishaji na waagizaji binafsi kuzalisha na kuagiza sukari.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo ,Februari 8,2023 na Mkurugenzi Mkuu NSSF,Masha Mshomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko na mwelekeo wa utendaji katika mwaka wa fedha 2022/23.

Mshomba amesema kuwa Mradi huo unatarajiwa kutoa fursa ya soko kwa wakulima wa nje wanaolima miwa katika mashamba yenye takribani hekta 450, miundombinu mingine kwa ajili ya wananchi wanaouzunguka mradi huo,ajira zaidi ya 2,315 za moja kwa moja, megawati 15 za umeme zinazotarajiwa kuingizwa katika gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupokelea na kupoza umeme Msamvu.

“Mradi huu unatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka na umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na uzalishaji wa sukari kuanza Julai, 2023,”amesema Mshomba.

Aidha ameeleza kuwa mfuko huo katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, unatarajia kukusanya michango ya shilingi trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya shilingi trilioni 1.4 iliyokusanywa na Mfuko katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha, kuendelea kumudu gharama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine,

“Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, Mfuko unatarajia kulipa mafao yenye thamani ya shilingi bilioni 769.3 ambayo ni ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na shilingi bilioni 659.8 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022,”amesema Mshomba

Akizungumzia mafanikio ya mfuko huo Mshomba ameeleza kuwa ukuaji wa Mfuko kwa Kiwango Kikubwa Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko umekuwa kwa kiasi kikubwa ambapo thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi trilioni 6.6 mwezi Desemba 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 39 kutoka shilingi trilioni 4.7 iliyofikiwa mwezi Machi 2021.

“Ongezeko hili lilitokana na kuongeza kwa michango ya wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji,Ukuaji huu wa Mfuko unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu kwa ajili ya utoaji huduma za Hifadhi ya Jamii na Michango ya wanachama 2022/23 inatarajiwa kufikai shilingi trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya shilingi trilioni 1.4 kwa mwaka 2021/22.