May 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nsekela aeleza mafanikio miaka 30 Benki ya CRDB

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema hatua ya kuanzishwa kwa CRDB (1996) Limited, ambayo iliendelea kufanyiwa mageuzi na baadae kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2009 na kujulikana rasmi kama CRDB Bank Plc, ilikuwa hatua ambayo imefungua ukurasa mpya wa mafanikio hadi sasa ikiwa ni moja ya benki bora na kiongozi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mafanikio haya tunayoshuhudia leo katika miaka 30 ya uongozi kwenye Sekta ya Fedha hayakuja kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati katika teknolojia. Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi ya kiteknolojia kwenye sekta ya benki, jambo ambalo limekuwa nguzo muhimu ya mageuzi yao,”amesema.

Ameyasema hayo Mei 16, 2025 kwenye Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika Ukumbi wa Simba katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt.Philip Mpango.

“Mwaka 1999, Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza nchini kutumia mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa kibenki (core banking system), hatua iliyotufanya tuunganishe matawi yetu yote chini ya dhana ya ‘One Bank, One Branch.’ Kabla ya hapo, kila tawi lilifanya kazi kama benki tofauti, jambo ambalo lilifanya huduma kuwa na changamoto nyingi.

“Mageuzi haya ya kiteknolojia yaliambatana na mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya matawi yetu na kuweka vifaa vya kisasa ili kuendana na maendeleo ya kidijitali. Ni katika msingi huu wa uwekezaji katika teknolojia, katika miongo hii mitatu, benki yetu ya CRDB si tu imekua kufikia kuwa benki kiongozi nchini, lakini pia imebadilisha maisha ya watu na uchumi”amesema Nsekela.

Nsekela amemueleza Makamu wa Rais kuwa azma ya benki hiyo daima imekuwa ikiboresha maisha ya watu na kukuza uchumi kwa ujumla. Ili kutimiza hilo, wameweka mkazo kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa na mikakati madhubuti inayowawezesha kuwafikia wananchi mijini na vijijini kwa ufanisi zaidi.

“Tangu mwaka 1996 tulipoanza safari yetu mpya tukiwa na matawi 19 pekee, tumeendelea kupanua mtandao wetu hadi matawi 260 kote nchini. Mageuzi haya yameambatana na uwekezaji mkubwa kwenye mifumo ya kidijitali.
Tukiongozwa na kaulimbiu ya ‘Benki inayomsikiliza mteja’, tumekuwa vinara wa kuanzisha asilimia 95 ya suluhisho za kibenki zinazotumiwa sokoni. Huduma kama TemboCard, ATM, na PoS (2002), SimBanking (2011), na CRDB Wakala (2013), zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya fedha na kuchochea kasi ya ujumuishi wa kiuchumi.

“Zaidi ya teknolojia, tumeendelea kubuni huduma mahsusi kwa makundi mbalimbali, kunzia watoto, wanafunzi, wafanyakazi, wastaafu, wajasiriamali na kampuni na taasisi. Mwaka 2016 tulikuwa Benki ya kwanza nchini kutoa huduma za bima kabla ya kuanza kwa mfumo wa Benkibima (BancAssuarance), baadae mwaka 2021 tulianzisha huduma zinazofuata misingi ya sharia ‘CRDB Al Barakah’. Haya yote ni sehemu ya dhamira yetu ya kujenga benki bunifu na jumuishi,”amesema Nsekela.

Nsekela amesema, Benki ya CRDB inajivunia kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Sera za Mazingira, jamii, na Utawala Bora (ESG). Mwaka 2019, walikuwa benki ya kwanza nchini kupata usahili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UN-GCF). Ni katika muktadha huo, walikuwa wa kwanza nchini kutoa Hatifungani ya Kijani (Kijani Bond). Na mwishoni mwa mwaka jana kwa kushirikiana na TARURA walitoa Hatifungani ya kwanza ya Miundombinu ya Barabara nchini (Samia Infrastructure Bond)..

Amesema kwa miaka 30 ya ukuaji, teknolojia imeendelea kuwa nguzo ya mafanikio ya Benki ya CRDB ndani na nje ya Tanzania. Mwaka 2012, walivunja rekodi kwa kuwa benki ya kwanza ya Kitanzania kupanua huduma nje ya mipaka kupitia CRDB Bank Burundi, ambayo leo inaongoza katika kukuza ujumuishi wa kifedha nchini humo.

“Mwaka 2023 tuliingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), soko lenye fursa kubwa, na pia tukawa Benki ya kwanza kuanzisha kampuni tanzu ya bima, CRDB Insurance, pamoja na taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuthibitisha dhamira yetu ya kuwa daraja la maendeleo barani Afrika.

“Leo hii, Benki ya CRDB ni benki kubwa zaidi nchini kwa mizania, ikiwa na mali za zaidi ya sh. trilioni 16.6 kwa mwaka 2024. Tunaongoza kwa amana za wateja (sh. trilioni 10.9) na utoaji wa mikopo (sh. trilioni 10.4), tukithibitisha imani ya wateja na mchango wetu mkubwa katika kufadhili maendeleo ya sekta binafsi na ya umma ndani ya Afrika Mashariki na Kati.

“Faida baada ya kodi ya sh. bilioni 551 kwa mwaka 2024 ni ushindi mkubwa ukilinganisha na hali ya hasara mwaka 1996. Ukuaji huu umeendelea kuwanufaisha wanahisa wetu, wakiwemo Serikali, kupitia gawio la kila mwaka. Benki ya CRDB pia imekuwa miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini, ikitambuliwa na TRA, ikiwa ni uthibitisho wa uwajibikaji wetu kwa taifa na dhamira ya kuleta mafanikio ya pamoja” amesema Nsekela.

Nsekela amesema Benki ya CRDB wanaamini kuwa uwepo wao ni kwa ajili ya kutoa mchango endelevu wa kuboresha maisha ya watu na jamii inayowazunguka. Kupitia sera yao ya uwekezaji kwa jamii inayoelekeza asilimia moja ya faida kurudishwa katika jamii, hivyo kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita ilikuwa imejikita katika maeneo ya elimu, afya na mazingira.

“Katika Sekta ya Elimu tumewezesha ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, maktaba katika shule za msingi na sekondari sambamba na utoaji wa vifaa vya masomo pamoja na madawati, ambapo kwa mwaka 2024 pekee tuliwekeza zaidi ya sh. milioni 350 kupitia kampeni yetu ya “Keti Jifunze”. Na leo hii, tukiwa tunasherehekea miaka 30 tokea kuanzishwa kwa benki yetu tunakwenda kuzindua mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano itakayojengwa katika Manispaa ya Ilala (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam). Mradi huu unaonesha dhamira yetu ya kudumu ya kuwekeza katika mustakabali wa vijana wa Tanzania kupitia elimu bora.

“Ninajivunia kukujulisha kuwa katika safari hii ya miaka 30, benki yetu imekuwa ikitambulika kama ‘Kitovu cha Ubora’, ikitajwa kuwa Benki Bora Tanzania katika tuzo mbalimbali za kimataifa ikiwamo tuzo katika tuzo kubwa zaidi za ‘Euromoney’,‘Global Finance,’ ‘The Banker’, na zile zinazotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya (European Society for Quality Research-ESQR). Katika kipindi cha miaka hii 30, benki yetu imetunukiwa zaidi ya tuzo 170, na bado zinaendelea kuja.  Hii inadhihirisha ubora wetu katika nyanja mbalimbali za kiutendaji. Tunajivunia sana mafanikio haya” Nsekela amemueleza Makamu wa Rais.