Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Arusha
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela ametangaza mikakati ya kuifanya benki hiyo kutoa huduma bora pamoja na kuona kampuni zote tanzu zilizo chini yake zinaendeshwa kwa tija kwa kuzalisha faida.
Pia kukuza mtaji wa benki hiyo utakaowezesha kufungua matawi kwenye nchi nyingi zaidi za Afrika na kutoa huduma za kifedha kwa kujitofautisha na taasisi nyingine za kifedha ambapo mpaka sasa wana matawi nchi za Burundi na Congo DRC.
Ameyasema hayo Mei 18, 2024 wakati anatoa taarifa yake ya utendaji kwa mwaka 2023 kwenye Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC)
“Jambo la msingi lazima tujitofautishe na benki nyingine na watoa huduma wengine kwa kutoa huduma yenye ufanisi, huduma yenye kipaumbele, huduma inayomfanya mteja afurahie huduma zetu.Tutaendelea kuwa wabunifu na kuleta mabadiliko makubwa na mtaendelea kuyaona ndani ya benki yetu,”amesema Nsekela.
Nsekela amesema jambo jingine ni kuwa karibu na jamii hivyo lazima washirikiane nayo ili kuleta mabadiliko na kila wanachokifanya kioneshe mafanikio kwa wananchi wanaowazunguka huku imani yake ni kwamba wakifanya hivyo kupitia kampuni zao tanzu, watawafikia wengi zaidi.
“Unapoongeza uendeshaji lazima uangalie milango ya viashiria hatarishi,lazima tuongeze usimamizi maeneo tutakayoelekeza nguvu zetu kwanza ni kuhakikisha kwamba sheria (za nchi) zinapoendelea kutungwa na benki yetu inaendelea kuwa imara,”ameeleza.na kuongeza kuwa
“Jambo jingine ni mtaji uliopo unatunzwa, na unaongezeka pasipokuathiri uwekezaji, lazima tujipambanue kama benki yenye TEHAMA ya kisasa na inayotumia zaidi mabadiliko ya teknolojia hapa nchini na nje ya nchi,”.
Nsekela amesema kama benki, wanaamini utawala bora hivyo wahakikishe wanatoa taarifa kwa uwazi, ubora na zilizo sahihi pamoja na kuhakikisha taarifa zao zinawafikia walengwa kwa muda sahihi ili kujilinganisha na nchi za dunia ya kwanza.
Ameongeza kuwa, benki yao lazima iendelee kuwa kinara wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kujihusisha na utunzaji wa mazingira na kupitia jambo hilo nchi ya Tanzania imewatambua, na dunia imewajua.
Hivyo CRDB ipo tayari kuwawezesha kifedha watu wenye asasi na vikundi vya kushughulika na utunzaji wa mazingira pia kuna fedha kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula hasa mahindi.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya