Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya NMB imekabidhi msaada wa mabati 600, madawati 100, pamoja na viti 50 na meza 50, kwa ajili ya shule nne za Msingi na Moja ya Sekondari, zilizopo Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam, vyote vikiwa na thamani ya Sh.Mil.39.
Hafla ya makabidhiano hayo yamefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sekondari Kibasila, huku shule za msingi zilizonufaika na msaada huo zikiwa ni Keko Magulumbasi, Mtoni, Azimio na Chemchem.
Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard alimkabidhi misaada hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.
Donatus alisema wakati wa hafla hio, thamani ya msaada huo ni sehemu tu ya Sh. Bilioni 2, ambazo ni sawa na asilimia 1 ya faida ya NMB kwa mwaka uliopita wa 2021, kwa kupitia Sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika Sekta za Elimu, Afya na Majanga mbalimbali.
Meneja huyo aibainisha kuwa, Kibasila imepokea viti 50 na meza 50, huku shule za msingi Keko Magulumbasi, Azimio ya Tandika na Mtoni ya Mtoni kijichi kila moja ikipewa mabati 200, wakati Shule ya Chemchem ya Mbagala ikijipatia madawati 100.
Aidha, Rugwa aliipongeza NMB kwa namna inavyoijali jamii kwa kushirikiana bega kwa bega na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kwa kuboresha mazingira ya kujisomea, kufundishia, na upatikanaji wa huduma za afya ndani ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
“Hakika NMB ni mshirika sahihi sio tu wa harakati za maboresho ya mazingira ya kujisomea na kufundishia, bali na suluhishi mbalimbali za kifedha. Kila yanapotokea mahitaji, NMB haijawahi kusita kuisapoti jamii inayoizunguka,” Rugwa aliongezea.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati