January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatoa msaada wa madawati 100 Bunda

Raphael Okello, Timesmajira Online,Bunda.

MKUU wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Naano amepokea madawati 100 yenye thamani ya milioni 12 yaliyotolewa msaada na benki ya NMB kwa ajili ya Shule ya msingi Nyasura katika Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara.

Shule ya msingi Nyasura ni moja ya Shule inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati kutokana pia uwepo wa wanafunzi wengi.

Viongozi wa NMB na serikali wakikabidhiana madawati katika Halmashauri ya Mji wa Bunda

Akipokea madawati hayo Mkuu huyo wa Wilaya amesema shule za Bunda bado zina upungufu mkubwa wa madawati 16000 ambapo Halmashauri ya Mji wa Bunda ina upungufu wa madawati takriban 6000 na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina jumla ya upungufu wa madawati zaidi ya 10000.

Dkt.Naano ameipongeza benki ya NMB Kwa kuchangia madawati 100 na mbunge wa Jimbo la Bunda mjini, Robert Maboto kuchangia madawati 1049 kupitia mfuko wa Jimbo .

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameiomba NMB kuendelea kujitolea zaidi ikiwezekana kuongeza idadi ya madawati Ili kukabiliana na changamoto hizo wilayanzima.

Amewataka Madiwani kuandaa utaratibu mzima utakaowafanya wazazi na walezi Bunda nzima kuchangia madawati angalau dawati moja Kwa wazazi watatu.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali na Binafsi NMB tawi la Bunda William Makoresho amesema benki hiyo ipo katika mwendelezo wa kutoa huduma Kwa jamii hususani sekta ya elimu kwa kuchangia uhitaji na itaendelea kutenga bajeti kwa ajili kusaidia jamii.

MKUU wa taasisi za serikali na binafsi wa NMB tawi la Bunda William Makoresho

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Emanueli Mkongo amesema shule zenye upungufu mkubwa wa madawati ndani ya halmashauri ni pamoja na shule ya msingi Bigutu ikifuatiwa na shule ya msingi Nyasura.

Mkongo amesema katika kukabiliana na upungufu huo watakuwa wanagawa madawati kadri ya uhitaji wa shule na namna yatavyokuwa yanapatikana.

Amesema kutoka na makusanyo ya ndani halmashauri yake inaendelea kutengeneza madawati zaidi katika kukabiliana na changamoto hizo.

Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza NMB na Mfuko wa Jimbo kwa kuchangia halmashauri katika juhudi za kukabiliana na upungufu wa madawati huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu kufikia malengo .

Mkongo amesema halmashauri hiyo imepata kiasi cha fedha takribani milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ambapo shule hiyo ya Nyasura ni moja ya shule ambayo itagawanywa kutokana ujenzi huo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Emmanuel Mkongo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.

Akiongea Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bunda, Robert Maboto,Katibu wa Mbunge Emmanuel Kija amesema Mbunge huyo,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na ofisi ya Mkuu wa Wilaya wameadhimia kushirikiana na wadau wengine kupunguza adha ya madawati katika shule za msingi na sekondari katika jimbo hilo.