January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatoa msaada wa bati 200 Muheza

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Muheza

BENKI ya NMB imetoa msaada wa bati 200 zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 8,000,000 kama mchango wake kwa jamii kwa shule nne za msingi za Mtindiro, Bwitini, Songa na Kilulu katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Akizungumza leo Juni 14, 2022, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Dismas Prosper alisema kila shule itapata bati 50 kwa ajili ya kupaua vyumba vya madarasa ambavyo kwa kiasi kikubwa vilijengwa kwa nguvu za wananchi.

“Benki ya NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii. Ni kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia moja ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka.

“Kwa taarifa tu, Benki ya NMB imetenga zaidi ya sh. bilioni mbili kwa mwaka huu 2022 kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali kwa jamii zetu katika maeneo niliyoeleza hapo awali. Shule na vituo mbalimbali vya afya nchini kote vitanufaika na vifaa mbalimbali kwa mwaka huu, na endapo yataibuka majanga (japo hatuombei), Benki ya NMB itasimama pamoja na wahanga katika kipindi hicho” alisema Prosper.

Prosper alisema kiasi hicho kilichotengwa kwa ajili ya jamii kinawafanya kuwa benki inayochangia kiasi kikubwa zaidi kwa jamii kwa hapa nchini Tanzania.

“Kwa taarifa tu, Benki ya NMB ndiyo benki inayoongoza nchini huku tukiwa na matawi 226, mashine za ATM zaidi ya 800 nchi nzima, NMB Wakala ni zaidi ya 10,000 pamoja na wateja ni zaidi ya milioni nne (4), idadi ambayo ni hazina kubwa ukilinganisha na benki nyingine hapa nchini.

“NMB imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100, na tunaendelea kuboreshs huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ili kuwafikia wateja wengi zaidi kwa njia rahisi na salama. Na Benki ya NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa katika kuhakikisha kuwa changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi katika kuboresha huduma za elimu” alisema Prosper.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza Halima Bulembo, aliishukuru benki ya NMB kwa kusema msaada huo utakuwa ni mkombozi kwa shule hizo, huku akitanabaisha kuwa bado changamoto ni kubwa ya vyumba vya madarasa, kwani wilaya ina kata 37, na wangependa kata zote zipate msaada huo.

Bulembo alisema Benki ya NMB imekuwa ikijitoa kwa hali na mali katika kuisaidia jamii, kwani walishafanya hivyo siku za nyuma, na anaamini wataendelea kutoa msaada huo kwa maeneo mengine siku zijazo, huku akishukuru Benki ya NMB kupokea maombi yao kupitia Meneja wa Tawi la NMB Muheza Anna Chimalilo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwao kuona wanapata msaada kutoka Benki ya NMB.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Erasto Mhina alisema msaada huo utawaongezea ari ya kusoma wanafunzi, na kuweza kufanya vizuri kwenye masomo yao. Lakini pia akawaomba Benki ya NMB kuweza kuisadia shule ya kihistoria ya Magila, ambapo ndipo chimbuko la elimu kwa nchi ya iliyokuwa Tanganyika.

“Tunaomba muitupie macho Shule ya Magila. Shule hii kongwe, ni ya kihistoria yenye miaka zaidi ya 100. Ina hali mbaya, hivyo ninyi kama NMB, mnaweza kuienzi Wilaya ya Muheza ambayo ndiyo chimbuko la elimu nchini.

“Pia kutokana na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia, Benki ya NMB mnatakiwa sasa kufikiria kutoa kompyuta na printa kwenye shule zetu. Nina hakika vifaa hivyo vitasaidia watoto wetu kufaulu vizuri” alisema Mhina.

Mhina amemshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kujali watoto wote wa kike na wa kiume kupata elimu, ambapo amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, na Wilaya ya Muheza ni moja ya wanufaika wa kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Halma Bulembo (kulia) akizungumza kwenye hafla fupi iliyofanyika Kijiji cha Kilulu kabla ya Benki ya NMB kumkabidhi bati 200 zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 8,000,000 kwa shule nne za msingi. Katikati ni Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Dismas Prosper, na kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Muheza Anna Chimalilo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Halma Bulembo (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa bati 200 zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 8,000,000 na Benki ya NMB kwa ajili ya shule nne za msingi. Hafla ya makabidhiano ilifanyika Kijiji cha Kilulu. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Halma Bulembo (kulia) akipeana mikono na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini Dismas Prosper (kushoto). Ni kwenye hafla fupi iliyofanyika Kijiji cha Kilulu, baada ya Benki ya NMB kukabidhi bati 200 zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 8,000,000 kwa wilaya hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).