Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar
BENKI ya NMB, kupitia Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), imetoa msaada wa viti na meza 150 kwa Shule Sekondari Saranga ya Kimara na Mashujaa ya Sinza, pamoja na mabati 175 kwa Shule ya Msingi Mianzini, iliyopo Magomeni Makurumla – zote wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 20.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Shule ya Sekondari Saranga, ambako Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Vicky Bishubo, alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James, mbele ya Mbunge wa Ubungo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Kitila Mkumbo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Bishubo amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wao wa kila mwaka, ambako hutumia asilimia moja ya faida yao kwa mwaka uliotangulia, kurejesha kwa jamii kwa kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta za Elimu na Afya, pamoja na majanga.
Bishubo amebainisha kuwa, NMB inatambua, kuthamini na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya vijana na watoto wa Kitanzania kupata elimu bora, hivyo wao kama wadau, wanao wajibu wa kusapoti jitihada hizo kwa kusaidia kila penye uhitaji.
“Tangu Januari mwaka huu hadi sasa NMB imetumia Sh. Bilioni 1.3 kutoa misaada, ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam Peke yakep benki imetoa misaada yenye thamani ya Sh. Milioni 207.9, kati ya hizo Sh. Mil. 144.5 katika elimu na Sh. Mil. 93 Sekta ya afya,” amesema Bishubo.
Kwa upande wake, DC James, ameishukuru NMB, aliyoitaja kama sehemu ya familia ya maendeleo wilayani mwake kutokana na ushiriki wao wa mara kwa mara wa utatuzi wa changamoto katika elimu na afya, huku akiwataka walimu na wanafunzi kutunza misaada hiyo, ili idumu kwa muda mrefu.
“NMB wamekuwa wanafamilia wa maendeleo Ubungo, tangu siku naapishwa walikuwa na sisi, naanza kazi NMB ilikuwa pamoja na sisi, tuliposimama kuhangaika na changamoto za sekta ya elimu na afya, NMB iko pamoja nasi. Wao wako na sisi katika raha na shida.
Naye Waziri Mkumbo, ameishukuru NMB kwa namna inavyosaidia jamii inayoizuguka na kwa kuhakikisha wanaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili jamii.
More Stories
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla