November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatenga Bilioni Moja kusaidia wabunifu wachanga

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imetenga Sh. bilioni moja kwaajili ya kuwasaidia wabunifu wachanga waweze kuimarika na kuzifanya bunifu zao kuwa bora na zenye manufaa kwa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Meneja Idara ya Utafiti wa Benki ya NMB, Prochest Kachenje alipokuwa anamuelezea Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga alipotembelea banda la NMB wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Tafiti na Ubunifu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.

“NMB imetenga shilingi bilioni moja kwaajili ya kuwasaidia wabunifu wanaochipukia kuweza kuziweka bunifu zao katika utekelezaji ili waweze kunufaika”

“Mwaka jana tulizindua mfumo maalumu wa NMB Sandbox Environment ambapo wabunifu wa suluhishi mbalimbali za kifedha wanaweza kufanya majaribio ya bunifu zao na kwa zitakazo fuzu, tutashirikiana nao,” aliongezea Prochest.

Lakini pia, Prochest alisema kuwa kiasi hiki cha fedha sio mkopo bali ni fedha iliyotengwa kwa dhumuni ya kusaidia wabunifu hawa na hawatawajibika kuirejesha.

Alitumia pia fursa hiyo kuwakaribisha wanachuo na Vijana wabunifu kuishirikisha Benki ya NMB juu ya bunifu zao ili kuwasaidia kupata fedha za kuboresha zaidi.

Meneja wa utafiti wa Benki ya NMB, Prochest Kachenje akizungumza na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga alipotembelea banda la NMB wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Tafiti na Ubunifu – Chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Maafisa wa benki ya NMB kwenye picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Tafiti na Ubunifu – Chuo kikuu cha Dar es Salaam.