Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar
BENKI ya NMB kupitia Kampuni ya Reliance Insurance, imewalipa bima ya Sh. Milioni 438.4 wafanya biashara 12 waliokata bima mbalimbali, kati ya waliounguliwa moto maduka yao katika Soko la Kariakoo, Julai 10 mwaka huu.
Hafla ya kuwakabidhi wafanyabiashara hao hundi yenye thamani hiyo, imefanyika Julai 27 katika Ofisi za NMB Kariakoo Business Center, ambako wahanga hao walikiri kuwa hasara na maumivu yao ya kuunguliwa yamepozwa na malipo hayo ya haraka ya bima.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi hundi ya mfano, Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya NMB, Martin Massawe, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni chanya wa kuzilinda kwa bima mali na pesa wanazotafuta kwa jasho lao, ili kuepuka maumivu yasiyo na mfarinji wakati wa majanga.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuwafuta machozi wafanyabiashara waliokata bima nasi kupitia mikopo yao ama waliokuwa na bima za mali bila mikopo, ambao walikuwa sehemu ya wahanga wa moto wa Julai 10 sokoni Kariakoo.
“Wito kwa Watanzania, moto wa Soko la Kariakoo uwe fundisho kwao juu ya umuhimu wa bima. Moto ama majanga huja bila kuyatarajia, unapokata bima unakuwa umejiwekea kinga kuilinda pesa ama mali uliyotafuta kwa jasho lako.
“Uwepo wa bima hukurejeshea nguvu haraka kana kwamba hakuna janga lililokutokea. Wito huu sio tu kwa bima za mikopo, bali mali zote kwani gharama za bima hizi ni nafuu mno,” alisema Massawe mbele ya wahanga hao 12 miongoni mwa waathirika wa moto sokoni Kariakoo.
Akisisitiza umuhimu na unafuu wa bima hizo, Massawe alitolea mfano wa bima ya moto kuwa hukatwa asilimia 0.25 ya thamani ya mali, na kwamba kama mali ya Sh. Mil. 100, makato yake ya bima ni Sh. 225,000 tu bila V.A.T kiasi ambacho ni rahisi kuliko bima za magari.
“Nyumba ya thamani ya Sh. Mil. 100, makato yake ya bima ni Sh. 150,000, sawa na 177,000 pamoja na V.A.T, hapa utaona ni kwa namna gani bima hizi ni nafuu, lakini zinazobeba nguvu kubwa majanga yanapotokea,” alisema Massawe, na kuongeza moto ulipotokea walikuwa wa kwanza kukimbilia ili kujua hasara za wateja wao.
Kwa upande wake, Joel Mwakalebela, ambaye ni Meneja Madai wa Kampuni ya Reliance Insurance, aliwapongeza wahanga hao kwa uamuzi wao wa kukata bima, huku akisisitiza Watanzania kutosubiri mikopo ili kukata bima, badala yake watumie huduma hizo ili kujilinda na majanga.
“Tukio la moto Kariakoo litufundishe kuwa bima sio tu ni kwa ajili ya pesa za mikopo, nenda kakate bima za moto, magari, nyumba, afya, mali na nyinginezo, kwa sababu majanga hayaepukiki, na pia yanapokuja hayapigi hodi kwetu.
“Tunawashukuru NMB kwa ushirikiano huu mwema uliowezesha malipo ya haraka kwa wahanga hawa. Wito wetu kwa Watanzania ni kutumia huduma zetu, ambazo zinapatikana katika kila tawi la NMB lilipo kote nchini,” alibainisha Mwakalebela.
Akizungumza katika hafla hiyo, Emmanuel Mbise, ambaye ni mmiliki wa maduka namba 019 na 026 yaliyoteketea kwa moto, alifichua kuwa maumivu waliyoyapata wahanga wa tukio hilo ni makubwa, lakini malipo ya bima kutoka NMB, yanawapa hafueni na faraja kubwa.
Mbise aliitaka Benki ya NMB kuongeza kasi ya kuwafikia Watanzania wa kada mbalimbali kote nchini kuwapa elimu ya bima, kwani alichogundua yeye ni kuwa huduma hizo ni nafuu sana, lakini uchache wa watumiaji wa bima nchini unatokana na wengi wa wananchi kukosa elimu.
Naye Sajida Kagasheki, ambaye pia ni mmoja wa wahanga, alikiri kupata faraja kubwa kupitia malipo hayo ya bimba, huku akiwataka Watanzania kukimbilia sana huduma za bima, ambazo ni mkombozi na mfariji wa kweli wakati wa matatizo kama ya moto, vifo, ulemavu, upotevu na kadhalika.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa