November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB ‘yakazia’ Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi Jumuishi kwa Wanawake


Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAFUNZO ya Uongozi na Usimamizi Jumuishi kwa Wanawake yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, yamefungwa Ijumaa Septemba 27, huku washiriki wakitakiwa kuweka alama chanya kwenye maisha ya wanaowaongoza, pamoja na kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao.

Mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanawake viongozi kutoka Taasisi za Umma, Taasisi Binafsi, Wizara na Idara za Serikali, Jeshi la Ulinzi wa Wanznchi Tanzania (WTZ) na Halmshauri, yalifungwa Afisa Mkuu wa Rasirimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akoonay akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Bi. Ruth Zaipuna.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Akoonay alisema anaamini mafunzo hayo yanaenda kuwa chachu ya kutengeneza viongozi bora zaidi miongoni mwa wanawake, na hivyo hayakuwa tu ya kuwajengea nyinyi uwezo, bali kuongeza amasa ya wanawake kuchangamkia nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali.

“Kupitia elimu mliyopata katika mafunzo haya ya wiki nzima, mmejengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazokwaza mchango wa wanawake katika ukuaji kiuchumi na uendelezaji wa taifa, tunajua mmepikwa na mmeiva tayari kwa majukumu kwenye taasisi zenu,” alisema

Akoonay akafafanua kuwa: “Dhana ya uongozi ni kuongoza wengine kufika mahali ambapo hawakuamini kama inawezekana, kwani mara nyingi inaaminika kuwa kiongozi unapaswa kuwa na dira na maono makubwa kuliko unaowaongoza

“Na kwa sababu hiyo, ili uwe kiongozi mzuri lazima ujifunze kuweka alama chanya kwenye maisha ya wengi, hususani unaowaongoza, mjifunze kuwapa watu nafasi ya kuonesha uwezo wao, pamoja na kuongezea uwezo walionao. Nawasihi nyinyi wote mkawe aina hiyo ya viongozi huko muendako,” alisema.

Alitoa wito kwa wanawake hao kuwa wasiache kujifunza, na kwamba mafunzo waliyopewa yameambatana na mifano na maelezo kutoka kwa viongozi mbalimbali, wakiwemo wanawake waliopigania uhuru, ambao wameacha vitabu na machapisho ambayo yana nyongeza ya kujifunza kwao.

“Mfano hai, mimi niko chini ya kiongozi mwanamke (Bi. Zaipuna), lakini kiutendaji shatumtazami wala kumuona kama ni mwanamke, bali ni kiongozi imara, shupavu na madhubuti, ambaye tukikaa kwenye mikutano inayojumuisha wanaume wengi, sauti yake ndio inayotuunganisha na kutupa dira ya pamoja,” alimaliza.

Kwa upande wake, Naomi Zegezege Mtemba aliyekuwa Mwenyekiti wa Wahitimu wa Mafunzo hayo, akitokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambako ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, aliishukuru Serikali kwa elimu kubwa waliyowapa.

“Kwa niaba ya wahitimu, tunawashukuru walimu na wakufunzia wa shule hii, lakini pia tunaishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa mpango madhubuti wa kutoa mafunzo mbalimbali ya kuwaongezea uwezo wanawake ili washiriki ngazi mbalimbali za uongozi.

“Mafunzo haya yametuwezesha kupata maarifa makubwa, ujuzi na uzoefu muhimu katika uongozi na usimamizi wa rasirimali watu, usimamizi wa majukumu yaliyo mbele yetu, usimamizi wa utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa na jamii.”

Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kabula Igambwa, alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga maeneo mbalimbali, ikiwemo Uzalendo, Maslahi ya Taifa, Usalama, Historia na Harakati za Ukombozi, Kuongeza uwezo wa Kufikiri Kimkakati na Misingi ya Uongozi.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni Kuongeza Ujuzi Binafsi wa Biongozi, Watu na Taasisi, Kuboresha Uwezo wa Kubadili Mawazo, Kukuza Utamaduni Jumuishi wa Taasisi, Kuongeza Uwezo wa Kutafuta Vyanzo vya Rasirimali Fedha, Kusimamia Kikamilifu Miradi ya Taasisi.

“Pia ni mafunzo yaliyoawapa nafasi ya Kuongeza Ujuzi wa Kuongza Taasisi Kimkakati, Utatuzi wa Migogoro, Masuala ya Itifaki, Kufanya Maamuzi Bora na Kujiandaa Kuchukua Nafasi za Juu Kiuongozi,” alibainisha Igambwa katika hafla hiyo.