January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yaipa kipaumbele Elimu ya fedha kwa vijana nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali chini ya Benki kuu ya Tanzania (BOT) waliweka kipaumbele utoaji wa elimu ya fedha kwa Watanzania hususani vijana kwa malengo ya kukuza jamii iliyo na uelewa na masuala ya fedha.

Kwa kutambua umuhimu huu, Benki ya NMB kupitia sera ya uwajibikaji kwa jamii, inatoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa makundi tofauti katika maeneo mbalimbali hapa nchini huku elimu ikielekezwa katika ufunguaji wa akaunti za Benki na utunzaji wa Akiba kwa manufaa ya baadae.

Katika ziara ya maafisa wa Benki ya NMB kwa mikoa ya Tabora, Kigoma na Shinyanga, mbali na kutembelea na kujionea namna Benki hiyo imekuwa chachu ya kukua kwa sekta ya Elimu na Afya nchini, walitumia fursa hii kutoa Elimu ya fedha hasa kwa wanafunzi.

Afisa wa benki ya NMB idara ya uwajibikaji kwa jamii, Aloyce Kikois, aliwasisitiza wanafunzi juu ya uwekaji wa akiba na kutumia Benki kama sehemu sahihi ya kuhifadhi fedha kwani ni salama zaidi.

Kwa mujibu wa Meneja wa Benki ya NMB idara ya Uwajibikaji kwa jamii, Lilian Kisamba alisema, Benki ya NMB tayari imetoa mafunzo hayo katika maeneo mbalimbali nchini huku zaidi ya watanzania 80,000 wakinufaika na elimu hii hasa katika ulimwengu wa sasa wa kiteknolojia.