November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yaimarisha mtaji wa rasilimali watu kupitia program ya Management Trainee

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Programu ya Benki ya NMB ‘Management trainee’ inayotoa mafunzo kazini kwa wahitimu wa vyuo vikuu umeiwezesha taasisi hiyo kuimarisha mtaji wake wa rasilimali watu na kuisadia kuwa muajiri bora nchini.

Hadi sasa programu hiyo iliyoanza takribani miaka 13 iliyopita imezalisha wataalamu wa maswala ya kifedha na kibenki zaidi ya 60.

Wanufaika nane wa uwekezaji huo walihitimu wiki jana jijini Dar es Salaam na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu.

“Ndoto zetu za kuwa wataalamu wa masuala ya kibenki leo imetimia. Tunaahidi kufanya kazi kwa nguvu zetu zote kama waajiriwa wa taasisi bora na kubwa ya fedha nchini Tanzania,” Bi Amanda Eseko alisema kwa niaba ya wenzake.

Aidha, aliongeza kuwa miaka miwili ya mafunzo mbalimbali waliyopitia haikuwa ya lelemama. Hata hivyo, alifafanua, miaka hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwao kwasababu wamejifunza mambo mengi na kupata fursa ya kufanya kazi NMB na kulihudumia taifa kwa ujumla.

Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa NMB, Bw Emmanuel Akonaay, alisema ana matumaini makubwa sana na vijana hao ambao hana shaka wataisaidia benki hiyo kuendelea kuwa kinara wa huduma za kifedha nchini.

“Kwa kipindi chote cha mafunzo yao, hawa vijana wameonyesha uwezo wa hali ya juu. Hii ni pamoja na kuweza kupata amana zenye thamani ya TZS bilioni saba na kusaidia kufunguliwa kwa akaunti mpya 5,000,” Bw Akonaay alibainisha.

Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mjumbe wa Bodi wa NMB, Bw Ramadhani Mwikalo, aliyesema kuwa uendelezaji wa vipaji kama huo ni moja ya vitu vinavyofanya NMB kuwa mwajiri bora na kinara nchini, na kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi na weledi mkubwa, ndiyo rasilimali namba moja ya benki hiyo na mtaji unayoifanya kuongoza sokoni.

Awali, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bw Filbert Mponzi, aliwaambia wahitimu hao kuwa kuajiriwa na mwajiri bora Tanzania ni kuwa sehemu sahihi na katika mikono salama kiajira.

Ili wafanikishe, alibainisha, ni lazima wazingatie kupata matokeo chanya katika kila wanalolifanya kwani hiyo ndiyo siri ya kufanikiwa kwa watu kama yeye ambao walianzia ngazi za chini walipoajiriwa NMB.

Wahitimu wa programu ya Management trainee wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NMB – Filbert Mponzi (kushoto), Mjumbe wa Bodi wa NMB – Ramadhani Mwikalo na Afisa Mkuu Rasilimali Watu – Emmanuel Akonaay (Kulia).