Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
BENKI ya NMB kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi wamezindua kampeni ya upandaji miti zaidi laki 2 na nusu katika kila mkoa ndani ya Kanda hiyo ili kuboresha mazingira.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Kazima, kata ya Ifucha katika Manispaa ya Tabora Afisa Mkuu wa Rasilimali watu wa Benki hiyo Emanuel Akonaay alisema kampeni hiyo imelenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini.
Alisema kama taasisi yenye dhamana ya maendeleo kwa wananchi inao wajibu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti na ili kuhakikisha kampeni hiyo iliyanzishwa na serikali inafanikiwa kwa asilimia 100.
Aliongeza kuwa katika kufanikisha kampeni hiyo wataendesha mashindano maalumu ya upandaji na utunzaji miti kwa shule za msingi ambapo washindi watapata zawadi za fedha taslimu na vyeti.
Akonaay alibainisha kuwa benki yake inatambua na kuthamini mazingira ndio maana wametenga kiasi cha sh bilioni 2 kutoka katika faida yao ya sh. bilioni 429 waliyopata mwaka jana, ili kufanikisha kampeni hii muhimu.
Aliongeza kuwa mwaka huu, Benki ya NMB inasherekea miaka 25 ya utoaji wa huduma hivyo wana kila sababu ya kurejesha shukrani kwa wateja wao ambao ni jamii na moja ya njia ya kusherekea ni kushiriki katika zoezi la upandaji miti miti ambapo matarajio yao ni kupanda zaidi ya miti milini 1 nchi nzima
Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Buriani, Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya aliaagiza Watendaji wa Mitaa, Vijiji, Kata na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo na kuhakikisha miti yote inayopandwa inatunzwa vizuri hadi ikue katika maeneo yao.
Alipongeza NMB kwa kushirikisha na TFS na wadau wengine kwa kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti ya asili zaidi ya 250,000 katika mikoa hiyo na kuitunza hadi ikue
Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mkoa kuendelea kuhifadhi, kutunza na kupanda miti kwa wingi ili kunusuru mazingira na uoto wa asili.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Misitu Kanda ya Magharibi Ebrantino Mgiye alisema kuna Kanda hiyo ina eneo lenye zaidi ya hekta mil 17.6 ambalo ni sawa na asilimia 35.5 ya misitu yote Tanzania Bara hivyo ni muhimu kuhifadhi bioanuai za mimea, wanyama na wadudu hapa nchini.
Aliongeza kuwa takwimu za kitaifa zinaonesha kasi kubwa ya kutoweka kwa misitu hapa nchini kwani takribani hekta 372,816 za misitu hutoweka kila mwaka.
Alitahadharisha kuwa vita kuu ya dunia ijayo itahusu maji hivyo kampeni hii ya upandaji miti kitaifa inalenga kuhakikisha nchi yetu na watu wake wanakuwa kwenye mazingira salama na ya uhakika kwa upatikanaji maji endelevu.
 Aliomba taasisi nyingine kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kulinda na kuhifadhi mazingira ili kulinda vyanzo vya maji vilivyopo kwa ustawi wa wananchi wake.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa