Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BAADA ya kuchanja mbuga mtaa kwa mtaa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Arusha, sasa Benki ya NMB imefika Mkoa wa Shinyanga kuzindua kampeni ya ‘Teleza Kidijitali’ katika mikoa ya Kanda ya Magharibi.
Uzinduzi huo ulifanyika katika viwanja vya CDT Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa Kanda ya Magharibi wa NMB, Sospeter Magesse alisema kampeni ya ‘Teleza kidijitali’ imeanzishwa hivi karibuni kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa huduma zilizo chini ya kampeni hio, ambazo ni NMB Pesa Wakala, Lipa Mkononi na Mshiko Fasta.
“Kupitia huduma ya Teleza kidijitali, pia inamuwezesha mteja kufungua akaunti mara moja na kuunganishwa na huduma za NMB Mkononi papo hapo bila mahitaji ya vigezo vingi vya usajili” alisema Magesse.
Aliongezea kuwa huduma yao ya ‘NMB pesa Wakala’ ni huduma inayomuwezesha mtu yeyote kuwa wakala kwa kupitia simu yako ya mkononi (smart phone au tochi) kutoa huduma za kuweka, kutoa au kutuma pesa kiurahisi.
Aidha, aliwasisitizia kuchangamkia fursa ya ‘Mshiko fasta’ ambapo mteja akiwa na akaunti ya NMB anaweza kukopa na kupata mkopo mpaka wa Shilingi 500,000/- bila dhamana na pia mteja atarejesha kidogo kidogo mpaka kwa siku 28.
“Kupitia huduma yetu ya Lipa Mkononi, mteja haendi na pesa katika kununua bidhaa bali ataskani QR code tu na kulipia. Hii inamuwezesha mfanyabiashara au mjasiriamali kulipwa pesa za mauzo moja kwa moja katika akaunti yake kiurahisi na kwa usalama bila kulazimika kuhamisha fedha nyingi kutoka eneo lake la biashara kwenda kwenye tawi” alisema Magesse.
Naye, mfanyabiashara mdogo wa kutoka kata ya Kahama mjini, Roseline Athuman amesema benki ya NMB imewaletea njia rahisi ya kufanya biashara na kuiomba iendelee kutoa huduma zao za kidijitali ili kuwarahisishia wafanyabiashara wadogo.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi